Breaking News

Ijue saratani ya damu (Leukemia) na tiba yake



 

 

Na Komba Kakoa

SARATANI  ya damu au Leukemia kwa jina la kitaalamu, ni hali ambayo mwili unatengeneza seli nyingi sana nyeupe za damu, kuliko kiwango ambacho kinatakiwa mwilini, seli hizi hutengenezwa na uvimbe kitaalamu kama tumour ambao unakua ndani ya mifupa ya kutengeneza damu.



Tabibu wa Tiba Asili na mbadala Othman Shem, kutoka Paseko Clinic iliyoko Tabata Relini jijini Dar es Salaam, anasema kuna aina mbili za saratani ya damu ambazo ni acute na chronic.

Anasema acute ni aina ya saratani damu ambayo seli nyingi nyeupe za damu ambazo hazijakomaa hutengenezwa ndani ya mifupa (bone marrows), na kuongezeka kuwa nyingi sana hivyo huzuia mifupa kutengeneza seli zingine za kawaida.

“Mara nyingi saratani ya aina hii huwapata watoto wadogo, japokua wakubwa pia wanaweza kupata ambapo inatakiwa watibiwe haraka ili kuepukana na vifo vinavyotokea ndani ya miezi tangu mtu kushambuliwa na tatizo hilo,” anasema.

“Chronic leukemia ni aina ya pili ya saratani ya damu ambayo hutokea pale mifupa (bone marrows) inapotengeneza seli nyingi nyeupe ambazo zimekomaa.

Anaongeza kuwa aina hii huchukua miezi au miaka kusambaa mwilini na matibabu yake hucheleweshwa mpaka mgonjwa atakapoonekana anafaa kuanza matibabu.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, jumla ya watu 24,500 wamefariki ambapo kati yao 14,300 ni wanaume na 10,200 ni wanawake mwaka 2017.

Mwaka 2009 hadi 2013, vifo vilivyotokana na leukemia vilikuwa vingi kwa wanaume na pia vilishika namba sita kwenye orodha  vifo vilivyoua wanawake zaidi ya saratani nyingine.

Aidha WHO linasema vipimo vya saratani kwa mwaka huu vinaonesha kuwa asilimia 10.2  ya wagonjwa wapya 1,688,780 wanasumbuliwa na saratani ya damu nchini Marekani.

Aidha kwa mwaka uliopita zaidi ya watu 1,290,773 walibainika kuwa na saratani ya damu

Kipindi cha miaka mitano tangu mwaka 1975 hadi 1977, kulikuwa na wagonjwa wa saratani ya damu kwa asilimia 34.2.
Na kuanzia mwaka 2006 hadi 2012, kulikuwa na asilimia 62.7, ambapo asilimia 94.1 walikuwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano na asilimia 93 ya watoto wenye umri chini ya umri wa miaka 15.

CHANZO

Kwa upande wake Salehe Mgonza kutoka Hospitali ya Kairuki jijini Dar es Salaam anasema kuna mambo ambayo yanaweza kuchangia kuanza saratani ya damu ikiwa ni pamoja na kupigwa na mionzi ya jua au x ray za hospitali ambayo kwa namna moja ama nyingine huharibu uwezo wa mwili kuamua ni kiasi gani cha seli kitengenezwe kwa wakati gani.

“Pia dawa zinazofanya kazi kwenye seli ambazo pia nyingine ni za kupambana na saratani zikiwamo methotrexate husababisha tatizo hilo,”anaongeza Dk. Shem

Dk. Mgonza anasema mtu akivuta au kugusa hewa ya kemikali ya benzene ambayo hutumika viwandani na kwenye sigara na kiasi kidogo kwenye mafuta yanayotumika kwenye gari, mifuko ya plastiki, gundi na rangi za kupaka mbao za viti na makabati anaweza kupata ugonjwa huo.

Aidha, kushambuliwa na baadhi ya virusi wajulikanao kama htlv huweza kusababisha saratani ya damu.

“Hata mtu kama kinga ya mwili wake umeishiwa kinga kuna uwezo wa kupata tatizo hilo kwani kinga ya mwili hupambana na kumaliza matatizo na kasoro zinazojitokeza kwenye mwili na kumuweka mbali na magonjwa,”.

Pia tatizo hilo hutokana na kurithi, kwani baadhi ya koo zina vimelea ambavyo hurithishwa kutoka wazazi kwenda kwa watoto, aina za saratani za kurthi ni mbaya sana kwani huweza kumaliza ukoo mzima.

“Matumizi ya kemikali za mbolea na kuulia wadudu shambani kitaalamu kama organophosphate huweza kusababisha tatizo hilo,”.


DALILI
Dk. Jason Yovandich, wa Shirika la Frederick National Laboratory (FNLCR) lililoko chini ya Taasisi ya Utafiti wa Tabia za Saratani nchini Marekani anasema dalili za acute leukemia ni kuishiwa damu, homa, kutokwa na damu sehemu mbalimbali kama puani, mdomoni, choo kubwa, machoni na matundu yote ya mwili, kupata maumivu kwenye mifupa na jointi za mwili, kuvimba maini, kuvimba bandama, kuugua mara kwa mara.

“Mara nyingi seli za saratani zikifika kichwani mgonjwa huanza kuumwa kichwa, kupata kizunguzungu, kichefuchefu na kutapika,

Dk. Yovandich anasema kwa upande wa chronic dalili zake ni kuchoka sana, kupungua uzito, kushindwa kupumua, maumivu ya tumbo, kutokwa jasho usiku, homa na moyo kukimbia, kuvimba kwa tezi, maini na bandama, kuishiwa damu, kinga ya mwili kushuka,” anaongeza.

TIBA MBADALA
Dk. Shem anasema ili kupambana na magonja ukiwamo saratani za aina mbalimbali mtu anatakiwa kutumia virutubisho vyote muhimu.

Anaongeza kuwa mara nyingi matibabu ya saratani yana madhara makubwa sana mwilini lakini mtu akitumia virutubisho vyenye vitamini mbalimbali huweza kumsaidia mgonjwa kupata nafuu na kupona haraka na kutopata madhara mengi.

“Virutubisho hivyo ni vile vyenye mchanganyiko wa vitamin nyingi ambazo kwa kawaida huzuia saratani ambavyo ni vitamin C, vitamin E, vitamin A na nyingine nyingi.

Virutubisho hivyo ni muhimu sana kwa wagonjwa wa saratani kutokana na ukweli kwamba wanakuwa na uwezo mdogo wa kula.

Matibabu ya saratani hii hutegemea aina ya saratani, kusambaa kwa saratani., umri na matibabu ya awali ambayo huhusisha dawa, mionzi, kuongezewa damu na kupandikiza.
Tiba hizi huwa ni kwa ajili ya kupunguza dalili, kuua chembe hai zisizo kawaida na kuongeza kinga ya mwili.

Kula lishe yenye mboga za majani na matunda itasaidia kukinga mwili na magonjwa na kuongeza damu, tumia mafuta ya samaki yana omega-3 fatty acid ambayo huzuia uzalishaji  wa chembe za damu zisizo kawaida kwa wingi na kuruhusu zile za kawaida kwa ajili ya kulinda mwili.

“Pata chanjo za mara kwa mara ili kuzuia maambukizi kwani saratani hii huvutia sana maambukizi kutokana na kushusha kinga ya mwili, fanya mazoezi mepesi mara kwa mara,”.

Kunywa juisi glass moja kila asubuhi itasaidia kuimarisha mwili na kuongeza kinga na uepukane na matumizi ya pombe, sigara na tumbaku.
========    



Maoni 3 :