Breaking News

Ajali za boda boda zinavyogharimu nguvu ya Taifa




Mwendesha pikipiki akiwa amepakiza abiria zaidi ya mmoja (Mishkaki kama inavyoonekana pichani
Na Komba Kakoa

UKOSEFU wa ajira na kutokuwapo  vyuo vya ufundi katika Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, ni jambo linaliosababisha vijana wengi kujihusisha na uendeshaji wa pikipiki.
 Kutokana na hali hiyo, vijana wengi wanaomaliza elimu yao ya msingi na sekondari hujikita katika biashara ya hiyo inayofahamika sana kwa jina la Bodaboda.
Pia inaelezwa kwamba ugumu wa maisha huchangia kwa kiasi kikubwa kwa vijana wenye umri mdogo kujiingiza kwenyeb biashara hiyo bila kuwa na elimu ya usalama barabarani licha ya kuwa ni hatari.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya umebaini kuwa, vijana hao ni wale wenye umri wa kuanzia miaka 14 na kuendelea ambao wengi wao hawazijui sheria na taratibu za barabarani.
Hiyo inatokana na vijana hao kujifunza kuchochoroni kwa kulipia kiasi cha shilingi elfu mbili kwa siku ambapo mafunzo hayo huchukua siku mbili mpaka tatu.
Pia imebainika kuwa vijana wengi wanaojishughulisha na kazi ya bodaboda ni wale walioshindwa kuendelea na elimu ya sekondari kutokana na sababu mbalimbali hususan changamoto za kimaisha.

Aidha wapo ambao wanafanya kazi hiyo kutokana na msukumo kutoka kwenye vijiwe ambavyo wamekuwa wakishinda kutwa nzima pamoja na rafiki zao wanaofanya kazi hiyo.

Juma Bakari(17), mkazi wa kijiji cha Dundani, ambaye ni miongoni mwa vijana wanaoendesha bodaboda anasema kuwa baada ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2015, hakufanikiwa kendelea na elimu ya sekondari, na kuamua kujiunga na kazi hiyo.
Bakari, anasema aliamua kujiingiza kwenye kazi hiyo baada ya kufundishwa na rafiki yake aliyekuwa naye kijiweni na kumlipa kiasi cha shilingi 4,000/ kwa siku mbili.
"Nilifundishwa na madereva wenzangu, siku mbili nikawa nimejua kuendesha vizuri, nikaanza kuomba bodaboda ili niweze kuifanyia kazi kwa lengo la kupata fedha za kujikimu na kusaidia wazazi wangu,''anasema.

pikipiki maarufu kama bodabpooda
Bakari, alifanikiwa kupata chombo na kuwekeana utaratibu na mmiliki kwa kupeleka shilingi elfu 7,000/ kila siku ambapo wameandikishiana mkataba ambao unawaongoza katika kazi hiyo.
Abuu Khalid (20),  ni mkazi wa kijiji cha Mkamba ambaye pia anajishughulisha na kuendesha bodaboda anasema chombo anachoendesha si mali yake ila ameingia mkataba wa makubaliano na mmiliki.
Anasema kuwa kujuana na rafiki ambao ni waendesha bodaboda ndio kumemfanya kujua kuendesha kwa kuwalipa kiasi cha shilingi 5,000/ ambao pia walimsaidia kupata chombo cha kuendesha.
Anaongeza kuwa amekubaliana na mmiliki wa chombo hicho kumpelekea kiasi cha shilingi elfu kumi, ambapo ameanza mwezi Januari mwaka huu ambapo ifikapo miezi 10, mkataba utafika ukomo na kumpatia fursa ya kumiliki chombo hicho.
"Ninaendesha bodaboda ya mtu kila siku napeleka shilingi elfu 10,000, ambapo kwa kipindi cha miezi 10 nitakuwa nimekamilisha kiasi cha shilingi milioni tatu na nitakabidhiwa usafiri huo ili uwe mali yangu,''anasema.



bodaboda ikiwa chini baada ya kupata ajali
Khalid, anasema kuna changamoto mbalimbali anazokumbana nazo ambazo ni baadhi ya wamiliki wa vyombo hivyo kutowajali pindi wanapopata ajali,huku mikataba yao ikiwataka kuwasilisha kiasi hicho cha pesa kila siku.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa kijiji Mkuranga, Dunia Said, anasema kuwa, makubaliano yaliyopo kati ya dereva na mmiliki ni kupeleka pesa kila siku lakini hakuna posho wala mishahara katika mikataba hiyo.
Nae, Mkuu wa usalama barabarani wilayani, Mkuranga Hamidu Mtinginjora, anasema ukosefu wa elimu ya usalama barabarani kwa madereva hao ndio chanzo cha kuwepo kwa ajali za mara kwa mara.
Anasema katika kipindi cha Machi hadi Mei mwaka huu, jumla ya ajali zilizotokea ni 10, na kusababisha vifo 16, majeruhi 10.

Anaongeza kuwa ajali hizo zimetokana na mishikaki, mwendo kasi na abiria kutovaa Helemet (Kofia ya kujikinga).

"Madereva wengi hawajui sheria za usalama barabarani, katika kubeba abiria zaidi ya mmoja, mwendokasi, kutofunga mkanda, kutovaa Helemet, mtoto kubebwa katika bodaboda au bajaji akiwa na umri chini ya miaka nane,''anasema.

Anasema kuwa katika makosa hayo kila kosa faini inalipwa shilingi elfu 30,000, lakini na wao wanatoza faini katika uvaaji wa kandambili kwa mwendesha bodaboda ambayo inakuwa shilingi elfu 30,000.
Anasema kuwa licha ya kuwatoza faini za mara kwa mara lakini bado tatizo ni kubwa kwani hakuna mabadiliko ambapo ajali zinaendelea kutokea  na kusababisha vifo na ulemavu wa kudumu.
Mtinginjora, anasema kuwa sheria inapaswa kufanyiwa marekebisho na kuongeza adhabu ziwe kubwa zitasaidia madereva kuwa makini jambo ambalo litapunguza ajali hizo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Elimu  ya Usalama barabarani Makao makuu ya Trafiki Dar es Salaam, Abel Swai anasema kipindi cha mwaka 2008 ajali nchini zilikuwa 2,036, vifo 309na majeruhi 1931.
Mwaka 2009 ajali zilikuwa 3406, vifo 508 na majeruhi 3,475 ambapo mwaka 2013, zilikuwa 6831, vifo 1,098 na majeruhi 6375.
Kadhalika mwaka 2014 zilikuwa 4169, majeruhi 3884, vifo 928 ikiwa mwaka 2015 ajali zilikuwa 2682,vifo 934 na kujeruhi 2370.
Pia kuanzia Januari 2016 hadi Machi mwaka huu ajali zilikuwa 663 na kujeruhi 200, ambapo vifo zilikuwa 559.

Kwa upande wa Afisa habari wa Kitengo cha Mifupa (MOI) Almas Jumaa, anasema kuwa kwa siku watu saba hufanyiwa upasuaji kutokana na bodaboda ambapo kati ya majeruhi wanaopokelewa asilimia 60 hutokana na bodaboda.

Anasema wahanga wa bodaboda ni vijana walio na miaka 18 hadi 40.
Aidha Jumaa, anashauri kwamba ifikie wakati kuanzishwe mazungumzo kati ya watu wa kampuni za bima za afya na hospitali ili kusaidia katika kutoa tiba kwa wagonjwa hao kutokana na mzigo mkubwa kuachiwa MOI pekee huku kampuni hizo zikichukuwa mamilioni ya fedha.

''Ajali zinapotokea asilimia 60 hawana uwezo wa kujitibu, hutibiwa kwa msamaha, lakini kampuni za bima zinanufaika pale ajali zinapotokea inatakiwa itengwe asilimia ambayo inapelekwa katika hospitali kutoka katika kwenye kampuni hizo,''anasema.

Hakuna maoni