Ziara ya Kinana 2014 na majipu ya Rais Magufuli
KATIKA moja
ya ziara za mikoani za kuimarisha chama, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Abdulrahman Kinana, aliwahi kuainisha upungufu katika utendaji wa
serikali na kueleza kuwa umesababisha wananchi kukilalamikia chama hicho.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akisalimiana a wananchi kwa bashasha, alipowasili katika kijiji cha Nyan'kanga, katika jimbo la Buanda mkoani Geita |
Hii ilikuwa
ni mwaka 2014 wakati akiitimisha ziara yake mkoani Singida kwa kufanya mkutano
wa hadhara kwenye uwanja wa Peoples na kusema kuwa watendaji serikalini
wamekuwa wakitumia ufumbuzi wa muda kama kuzima moto na akapendekeza kuwa lazima
tujenge utaratibu wa kumaliza matatizo ya wananchi uwe wa mipango ya muda
mrefu.
Kinana
aliutaja upungufu mwingine kuwa ni uwajibishaji wa watendaji wabovu, wakati
wanaharibu utawala bora haushiriki ila akishaharibu ndio utawala bora unaanza.
"Inaundwa
tume ya uchunguzi, kisa utawala bora, sipingi utawala bora bali napinga
unaolalia upande mmoja…dhambi kabla haijatendaka hatua hazichukuliwi ila
ukishakamilika ndiyo unachukuliwa,” akasema Kinana.
Katibu huyo
akakosoa utaratibu wa kuwahamisha watendaji wanaotuhumiwa kwa utendaji mbovu na
wizi, huku ikielezwa kwamba hakuna ushahidi wa kuwatia hatiani.
Akasema kuwa
ni lazima nidhami iongezeke serikalini, uwajibishaji, kuchukua hatua mapema na
kwamba imekuwa kawaida kwa jambo dogo kuachwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na
watu kwenye kituo kingine kabla ya kuchukuliwa hatua.
Nimejaribu
kueleza kwa kirefu kile ambacho Kinana aliwahi kukisema katika ziara zake kwa
lengo la kuelezea kile ambacho sasa kinafanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ya
Rais Dk. John Magufuli.
Ikumbukwe
kuwa mbali na hayo, Kinana aliwahi kuwaita baadhi ya watendaji wa serikali ya
awamu ya nne kuwa ni mzigo akawa anashauri waondolewe kwenye nafasi zao.
Katibu huyo
alikuwa akilalamikia udhaifu aliokuwa akiuona katika serikali hiyo na sasa
umeanza kushughulikiwa na Rais Magufuli na timu yake ili kurudisha nchi kwenye
mstari.
Ninaweza
kusema kuwa alichokuwa akikifanya Kinana ni kumuonyesha rais wa sasa majipu na
sasa anaendelea kuyatumbua kila anapoyabaini ili kuhakikisha hakuna malalamiko
ndani ya jamii kama huo ulioelezwa na katibu huyo.
Hata Makamu
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, (Bara), Philip Mangula, juzi aliweka wazi
kuwa kila anachokifanya Rais kina mkono wa CCM na anaunga mkono utendaji kazi
wa rais.
Waswahili
wana msemo wao usemao kuwa ukiona mwenzio ananyolewa na wewe tia maji, hivyo
wakati Rais Magugfuli akiendelea kutumbua majipu kwa watendaji wa umma, CCM nao
wajiandae kutumbuliwa.
Kwa sababu
anachokifanya kina mkono wa CCM kama alivyosema Mangula na pia hakuna siri
kwamba ndani ya CCM kuna majipu ambayo nayo yanahitaji kutumbuliwa ili chama
kirejeshe heshima yake mbele ya umma wa Watanzania.
Chama kuwa
na majipu siyo kauli yangu bali ni ya Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ambayo
aliwahi kuitoa mkoani Tanga kwamba kuna watu majipu ndani ya CCM ambao
wameficha makucha ili wasijulikane uovu wao.
Hilo Rais
Magufuli mwenyewe analijua kwa sababu alishawahi kusema kwamba ndani ya chama
hicho kuna watu wanafiki, ambao mchana wanakuwa CCM na ukifika usiku wanakwenda
upande wa wapinzani.
Mwisho.
Hakuna maoni