Breaking News

VIUNGO AU MWILI KUJAA MAJI ( EDEMA )


Na Komba Kakoa
EDEMA ni tatizo la viungo au mwili kujaa maji na kuonekana kama uvimbe kutokana na magonjwa ya moyo  ambayo husababisha ushindwe kufanya kazi zake vizuri hali ambayo husababisha damu kushindwa kufika katika maeneo mengine yakiwamo miguuni.
Hali hiyo husababisha mwili kukusanya na kuhifandi maji mengi zaidi ya mahitaji halisi na matokeo yake baadhi ya sehemu au mwili mzima hujaa na kuonekana kama umevimba.

Mbali na moyo kushindwa kufanya kazi yake, lakini pia matatizo ya mzio ‘Allergic Reactions’ yanaweza kuwa chanzo cha edema kwani kwa namna moja au nyingine inawezekana mwili umepatwa na chembe chembe ambazo haziendani na muundo mzima wa mwili.
Mfano wa chembe chembe hizi zinaweza kutokana na vyakula, mafuta ya kujipakaa au hata sumu baada ya kung’atwa na mdudu ambavyo vyote kwa pamoja husababisha mwili ujae maji hayo na kuwa katika muonekano wa uvimbe.
Christian Nordqvist ambaye ni mtaalamu wa masuala ya mfumo mzima wa mwili mwaka 2003 kupitia jarida la ‘Medical News’ aliandika kuwa magonjwa ya ini ( liver cirrhosis ), ambayo hupunguza utendaji kazi wa ini ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa vitu muhimu vinavyopatikana katika damu mfano protin (albumin) huweza kusababisha edema.

Anasema chanzo kingine ni pamoja na upungufu wa protini mwilini ambao husababishwa na matatizo ya kuwa na lishe duni au magonjwa ya ini, pamoja na magonjwa ya figo ambayo hupunguza utengenezaji wa damu mwilini kutokana na kuathiriwa kwa vitu muhimu katika figo vinavyohusika na damu ( erythropoietin ).

“Inawezekana mtu mwili wake ukajaa maji kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya mwili, mfano ni wamama wajawazito ambao baadhi yao huwa wanavimba miguu kutokana na miili yao kuwa na ongezeko la mahitaji ya damu ili kuweza kuutoshereza mzunguko mzima hadi kufika kwa kiumbe/viumbe walioko tumboni,”.
Mtaalamu huyo aliandika kuwa ngozi hujaa maji au kuvimba baada ya uwezo wa mishipa ya damu kuruhusu maji kupita ‘permiability’,  kubadilika ambapo mishipa hiyo ya damu huruhusu maji mengi zaidi yapite au yahame kutoka katika mchanganyiko wa damu na kuhamia katika tishu au nyama za mwili nje ya mishipa ya damu.
“Kwakuwa maji hayo hayapo katika mishipa ndio chanzo cha sehemu ya mwili kuonekana kama imevimba hali ambayo huruhusu kinga za mwili au seli zinazohusika na ulinzi wa mwili zifike kwa wingi zaidi katika sehemu hiyo na kupambana,”
Anasema mapambano hayo katika sehemu hiyo ni kwa lengo la kuziwezesha seli hizo zirejee katika utendaji kazi wake wa kawaida kutokana na maji hayo huwa na kiwango kikubwa cha seli zinazolinda mwili ambazo ni seli hai nyeupe za damu zinazofahamika kitaalamu kama leucocytes,”.

Anasema tiba ya tatizo hili hutofautiana kutokana na chanzo cha hali hiyo, hivyo matibabu hutofautiana hivyo ikiwa mtu atakumbwa na tatizo hili anatakiwa kufika katika kituo cha afya kilicho karibu iuli aweze kupata huduma.

TIBA
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2002 na Taasisi ya Tafiti za Magonjwa na Tiba asili ijulikanayo kama ‘European Histamine Research Society’, ulibainisha kuwa ili kutibu edema muathirika anatakiwa kuchua sehemu iliyoathirika.
“Kuchua sehemu hiyo kwa kutumia mafuta ya mzaituni ‘Olive  Oil’ kutasaidia uvimbe kupwaya na kushuka  kabisa hivyo mtu atapata nafuu na kupona kabisa.
Mbali na mafuta ya mzaituni lakini pia anaweza kutumia mafuta ya nazi ili kusugua taratibu sehemu yenye uvimbe, na ikiwa mwenye tatizo ni mjamzito massage ifanywe na mtaalamu wa tiba ‘Therapist’ ili kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza.

Maoni 1 :

  1. Nimeioenda makala hii ahsante kwa chapisho lako

    JibuFuta