MUHAS yafafanua matumizi ya dola
Na KOMBA KAKOA
LICHA ya Serikali kupiga marufuku matumizi ya fedha za
kigeni ikiwamo ‘dola’ lakini Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi
Muhimbili (MUHAS) kimeendelea na utaratibu huo.
Kutokana na hali hiyo Chama cha Wataalamu wa Maabara
Tanzania (MelSAT) kimeiomba Serikali ifuatilie suala hilo ambalo linadaiwa
kusababisha mkanganyiko miongoni mwa wataalamu hao.
Akizungumza na Mtandao huu hivi karibuni ofisini kwake, Makamu
wa Rais wa MelSAT, Peter Mwevila, alisema MUHAS imetangaza kozi ya kujiendeleza
ya Usimamizi wa Maabara (Laboratory Management) kwa wataalamu wa maabara lakini
malipo yameweka katika mfumo wa dola.
Hata hivyo alisema licha ya kozi hiyo kuwajumuisha
watanzania lakini malipo yake yanatakiwa kulipwa kwa mfumo wa fedha za kigeni.
“Kama wataalamu wa maabara ambao ndio walengwa wakuu katika
kozi hiyo lakini tunashangazwa na uongozi wa MUHAS kutaka wahitaji walipie mafunzo
hayo kwa mfumo wa dola,”alisema Mwevila.
Kwa upande wake Mohamed Zuber ambaye ni mtaalamu wa maabara alisema
kwamba ni kawaida kwa wataalamu wa fani mbalimbali kupatiwa mafunzo ama elimu
ya kujiendeleza lakini si kwa gharama kubwa kama iliyoainishwa na MUHAS.
“Ili mtu afanye kazi kwa ufanisi ni lazima apewe mafunzo ya kujiendeleza
na kupata maarifa mapya, lakini kama Mtanzania naona MUHAS hawajatutendea haki kuweka
ada kwa malipo ya dola angalau wangetuwekea kiwango kidogo katika mfumo wa
shilingi ili tujivunie chakwetu,”alisema Zuber
Kutokana na malalamiko hayo Mtandao huu ulimtafuta Afisa
Uhusiano wa MUHAS, Hellen Mtui, ambaye alikiri kuwepo kwa kozi hiyo na kwamba inatarajiwa
kuanza tarehe 12 Machi hadi 14 Aprili.
Alivyoulizwa kuhusiana na matumizi ya dola, Mtui alisema wanaolipa
kwa mfumo wa dola ni wale wanaotoka sehemu mbalimbali lakini kwa watanzania wanalipa
kwa shilingi.
Mtui alisema kwamba ni kozi fupi ya wiki tano kwa ajili ya
wafanyakazi kujiendeleza (Continues development course) na inajumuisha watu
kutoka sehemu mbalimbali.
“Kuhusiana na mfumo wa malipo ya fedha za kigeni ni kwa
ajili ya wageni kwani kuna fomu nyingine ambazo zimeandaliwa kwa lugha ya
Kiswahili kwa ajili ya Watanzania,”alisema Mtui.
Hata shivyo tangazo lililoshuhudiwa na Mtandano huu ambalo
limetolewa kwa lugha ya Kingereza na MUHAS linaonyesha ada ya mafunzo hayo ni 1500
ambayo ikikokotolewa katika viwango vya Shilingi ni 3,375,000.
Ikumbukwe tu kwamba mwaka jana Rais John Magufuli alipiga
marufuku matumizi ya fedha za kigeni huku Wazirin wa fedha Philip Mpango akibainisha
kuwa Januari moja mwaka huu ilikuwa ndio mwisho wa kutumia fedha hizo katika
huduma mbalimbali.
Aidha, Waziri Mpango alisema kwamba matumizi ya fedha za
kigeni humuumiza mteja lakini pia huathiri uchumi wa nchi.
Aliongeza kuwa suala la matumizi ya fedha za kigeni limeendelea
kuwa kero kwa wananchi kutokana na ugumu wa kusimamia matakwa ya sheria kwani baadhi
ya wateja hupewa kiwango cha thamani ya
kubadilisha fedha ambacho kiko juu kuliko thamani halisi iliyoko kwenye soko.
Mwisho.
Hakuna maoni