Maisha magumu yadaiwa kuchochea ongezeko la wagonjwa wa akili
Na KOMBA KAKOA
WATAALAMU wanafafanua kuwa ugonjwa wa afya ya akili (Kichaa) ni tatizo
kubwa linalowakumba watu wengi na kuathiri uwezo wa kufikiri, kudhibiti hisia
na tabia jambo ambalo huvuruga uwezo wao katika kufurahia uhusiano mzuri na
kukabiliana na changamoto za maisha.
Licha ya tatizo hili kuwa kubwa lakini linadaiwa kuongezeka kadri siku
zinavyokwenda kutokana na kuhusishwa na imani potofu huku waathirika
wakitelekezwa bila msaada wowote.
Ernest Mhusa ni Afisa Muuguzi katika fani ya Afya ya akili katika
hospitali ya Lutindi iliyoko Korogwe mkoani Tanga, anasema kuwa ugonjwa huo una
changamoto nyingi kutokana na ugumu wa maisha.
Dk. Mhusa anasema kuwa ugumu wa maisha humfanya mtu awe na msongo wa
mawazo na kujiingiza katika ulevi wa kupindukia, matumizi ya dawa za kulevya,
huku wengine wakirithi kutoka katika familia zao.
“Msongo wa mawazo husababisha matatizo ya Biochemistry kwenye
ubongo ambayo hifanya homoni ya Dopmini kupanda kiwango cha juu na kumfanya mtu
achanganyikiwe na kuzungumza mwenyewe huku akisikia kelele na sauti za watu
wasioonekana,” anasema.
Anasema kuwa mambo mengine yanayosababisha matatizo hayo ni migogoro
ya kifamilia, ndoa kuvunjika na matatizo mengine ambayo humfanya mtu kuwa na
msongo wa mawazo ambao wakati mwingine husababisha homoni ya Dopmini kushuka na
kuwa katika kiwango cha chini hivyo husababisha akate tamaa, kukosa amani na
wakati mwingine atamani kujiua.
“Kwasasa vijana ndio wapo kwenye hatari kubwa kupata matatizo haya
kutokana na matumizi ya vilevi kupindukia, dawa za kulevya aina ya Heroin,
bangi, na kutafuna mirungi na nyingine jambo ambalo humfanya kuwa na
hasira.”alisema.
Anaongeza kuwa kutafuna mirungi humfanya mtu akose usingizi jambo
ambalo husababisha apate matatizo ya Biochemistry ambayo humsukuma kufurahia
ama kusononeka wakati wote.
“Sababu nyingine ni kwamba kama mtu aliwahi kupata ajali anaweza
kutibiwa akapona au akaugua malaria kali (Celebral Malaria) na akatibiwa na
kupona lakini baada ya miaka kadhaa tatizo hilo linaweza kumpata,” anasema Dk.
Mhusa.
Anaongeza kuwa, kwa mtu ambaye aliwahi kupatwa na shida ya uti wa
mgongo na kutibiwa akapona pia yuko hatarini kupata shida hiyo.
Kwa upande wa Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitoa taarifa kuwa
magonjwa ya afya ya akili yanasababishwa na kushuka moyo, ugonjwa wa Schizophrenia na
kubadilika-badilika kwa hisia na kueleza kuwa yanayowadhoofisha watu wengi
ingawa huyapuuza huku wagonjwa wakiendelea kuaibika.
Kadhalika ripoti moja ya Shirika la Kitaifa la Magonjwa ya Akili
nchini Marekani inasema kwamba ingawa magonjwa ya akili yana tiba, lakini
nchini humo, takribani asilimia 60 ya watu wazima na karibia
asilimia 50 ya watoto wenye umri wa kati ya miaka 8 hadi 15 wanaougua
magonjwa ya akili hawakutibiwa katika mwaka uliopita.
TIBA YA UGONJWA WA AKILI
Katika kushughulikia matatizo ya afya ya akili mgonjwa anapaswa
kufuata matibabu yaliyopendekezwa na madaktari wa magonjwa ya akili ikiwamo
kufata ratiba maalumu atakayopewa na madaktari hao inayoeleza ni muda gani
mgonjwa anatakiwa kufanya mazoezi, kulala usingizi wa kutosha na wakati wa
kupumzika kila siku.
Pia kula lishe kamili, kuacha kutumia vilevi kupita kiasi, mgonjwa
anapaswa hushirikiana na watu anaowaamini na wanaomjali.
==============
Hakuna maoni