Mikorogo, lipustiki inavyoua watumiaji kimya kimya
Na Komba Kakoa
TAKWIMU zilizotolewa na Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) ya jijini Dar es Salaam, zinataja tatizo la saratani inayotokana na vipodozi imeongezeka kutoka wagonjwa zaidi ya 2,000 katika kipindi cha mwaka 2000 na kufikia 5,400 kwa sasa.Pia utafiti uliofanywa hapa nchini na Profesa Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Georgia, Atlanta, Marekani, Kelly Lewis wa kitengo cha Sosiolojia, kuhusu matumizi ya ‘mkorogo’ kwa wanawake nchini Tanzania, umebaini kwamba zaidi ya wanawake milioni sita wapo kwenye hatari ya kuugua saratani kutokana na matumizi ya vipodozi.
Kadhalika taarifa za utafiti huo zinaonyesha kwamba idadi ya wanawake wote Tanzania ni milioni 23 na kati yao asilimia 30 sawa na milioni 6 wanatumia vipodozi vyenye kemikali hatari na madini ya Zebaki, Hydroquinone pamoja na maji ya betri.
Kutokana na matumizi hayo, Lewis anasema Tanzania ipo kwenye hatari ya ongezeko la walemavu wa mtindio wa ubongo kwa wanawake wengi kuzaa watoto wakiwa kwenye ulemavu huo huku wengi wao wakipoteza maisha kutokana na kukithiri kwa matumizi ya vipodozi hivyo vilivyotengenezwa kwa kutumia kemikali zenye viambata sumu.
Zaidi Prof. Lewis anasema asilimia 70 ya vipodozi hivyo huingizwa kutoka nje ya Tanzania kupitia njia mbalimbali zikiwamo bandari bubu za Bagamoyo, Tanga pamoja na mipakani kwa kutumia usafiri wa malori makubwa ya mizigo ambayo hufanya safari zake katika nchi za Congo DRC, Kenya, Zambia, Malawi na nchi nyingine.
![]() |
Afisa habari wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFD) Gaudensia Simwanza akifafaniua jambo katika mkutano na waandishi hawapo pichani |
Ofisa Uhusiano wa TFDA, Gaudensia Simwanza anasema kuwa mamlaka hiyo imepiga marufuku vipodozi vyote vyenye viambata sumu, ingawa bado watu wanavitumia.
Katika kutokomeza matumizi ya vipodozi vyenye viambata sumu Simwanza anasema TFDA imeanza mpango wa kutoa elimu kwa wanafunzi ambao ni rahisi kuelimisha jamii kutokana na elimu watakayoipata.
“TFDA imebainisha baadhi ya vipodozi vyenye viambata sumu kuwa ni pamoja na Carolight, inayotajwa kuwa na sumu kali zaidi pamoja na vile vyenye madini ya zebaki au mercury sabuni ya jaribu na mekako clobetasol na betamethasone, krimu ya amira, betasol na skin success,”anasema.
Anasema tafiti za kitaalamu zimeonyesha athari kubwa ya matumizi ya kemikali hizo hasa kwa wanawake wajawazito kutokana na kemikali hizo kuathiri watoto wakiwa tumboni na kuwasababishia watoto hao ulemavu, saratani hata kifo mara wanapozaliwa.
Mkurugenzi wa idara ya kinga ya ORCI Dk. Julius Mwaiselage anaitaja kemikali nyingine ya Butylated hydroxyanisole (BHA) inayowekwa kwenye lipstiki kuwa husababisha saratani ya ini na figo. Pia Polyethylene glycols ambazo huwekwa kwenye krimu husababisha ugonjwa huo anasema.
Dk. Mwaiselage anasema changamoto kubwa ambayo wanakutana nayo ni hali ya wanawake wengi ambao hutumia vipodozi vilivyochanganywa kienyeji jambo ambalo ni vigumu kubaini aina halisi za kemikali zilizotumika ndani yake.
“Wanawake wanapaswa kuzingatia ushauri na elimu inayotolewa kuhusu hatari ya matumizi ya kemikali, kuachana na tabia ya kutumia vipodozi duni na kufuata maelekezo yaliyotolewa na TFDA ili kuepukana na matatizo ambayo siyo ya lazima,”anasema.
Dk. Tara Cullis kwa Canada ambaye ni muasisi wa taasisi ya David Suzuki Foundation ya chuo kikuu cha Harvard anasema kemikali ya BHA na Butylated hydroxytoluene BHT ni kemikali ambazo huwekwa kwenye lipsticks pia husababisha mtumiaji kupata saratani.
Mwalimu wa Shule ya Wasichana ya Kisutu jijini Dar es Salaam Daniel Kibona anasema ugonjwa wa saratani ya ngozi hauwezi kukoma hapa nchini kwasababu serikali haijaweka misingi imara ya kukomesha matumizi ya vipodozi vyenye viambata sumu.
Kibona anaongeza kuwa tatizo la matumizi ya vipodozi hivyo ni kubwa kwasababu halijaingizwa katika mitaala ya kufundishia wanafunzi na hakuna kipengele cha kufundisha juu ya madhara ya vipodozi kama ilivyo kwa magonjwa mengine ya malaria, kipindupindu, kichocho na mengine ya zinaa.
Naye mkazi wa Ilala Bungoni jijini humo, Zulfa Husein anasema chanzo cha utumiaji wa vipodozi hivyo ni tamaa inayosababishwa na wanawake wenyewe kuhamasishana kutumia mikorogo ili kutambiana urembo na kujikuta wakiharibu ngozi zao.
Rose Mkalimoto mkazi wa Kimara pia jijini Dar es Salaam anasema baadhi ya wanawake wanatambua madhara yatokanayo na matumizi ya vipodozi hivyo licha ya kupatiwa elimu mara kwa mara.
“Mimi niliwahi kumshauri mwanamke mmoja aache kutumia mkorogo, matokeo yake alikuwa mkali na kunikebehi kwa kuniita mshamba na ninamuonea wivu…hata ninapojaribu kuwaasa wasichana na marafiki zangu wengine hawanielewi kwasababu wameshajijengea kwamba uzuri wa mwanamke sharti awe mweupe ,” anasema Mkalimoto.
Anasema katika kipindi hiki pia kuna baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari ambao wamejiingiza kwenye matumizi ya vipodozi hivyo kutokana na kukosa elimu juu ya madhara ya vipodozi vyenye viambata sumu
Bahati Shukuru, ni miongoni mwa watumiaji wa vipodozi hivyo, anasema ni miaka mitano sasa anatumia vipodozi hivyo lakini ngozi yake inapendeza na kusababisha rafiki zake kuitamani kwa kiasi kikubwa.
“Mimi natumia na hata marafiki zangu wamevutiwa na weupe wangu, hayo madhara yanaletwa na watu wanaotaka kuvuruga biashara za wenzao mbona kuna watu wanaugua saratani ya ini, utumbo, na hata ya shingo ya uzazi nao wamepaka Carolite? anahoji Bahati.
Anasema wanaoumia ni wale wanaotumia mkorogo wa jadi: “Wanachanganya dawa ya meno na sabuni ya unga, jaribu pamoja na dawa ya kuondolea madoa kwenye nguo ‘jiki’,”anasema.
Dk.Elidje Ekra ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Treichville Abidjan, nchini Ivory Coast, anasema idadi kubwa ya wanawake wenye saratani ya ngozi nchini humo ilimfanya aamue kufanya utafiti uliogundua kwamba waathirika walikuwa wakitumia mikorogo ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kupata ugonjwa huo.
Anasema kuwa kemikali zinazotumika ili kuhakikisha ufanisi wa kuchubua rangi asili ya binadamu zinachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa matatizo ya shinikizo la damu pamoja na kisukari.
“Mikorogo inayochubua ngozi ni maarufu mno katika mataifa mengi ya Afrika huku wanawake wengi wakipendelea kujichubua ili waweze kukubaliwa kwamba ni warembo wanaovutia zaidi kumbe wanajitengenezea sumu inayowatesa na kuwamaliza kabisa,”anasema.
Anabainisha kuwa matumizi ya vipodozi hivyo yanachochewa na kasumba ya madai kwamba mwanamke mrembo sharti awe na ngozi laini na nyeupe, pamoja na kuwaridhisha wenzi wao wanaopenda wanawake weupe hali ambayo inazidi kuathiri wanawake kwa kiasi kikubwa bila wao wenyewe kujua.
Taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) inabainisha kuwa kati ya asilimia 100 ya dawa duniani kote 10 kati yake ni bandia au duni na kwamba asilimia 50 ya dawa hizo duni hutengenezwa kutoka nchini China na India ambako kuna maabara zilizoko chini ya ardhi.
Dawa hizo duni ni zile ambazo viambata vyake havikidhi viwango vya ubora vinavyokubalika kisayansi pamoja na mtengenezaji wake kubadili viambata, nembo, vifaa vya kufungashia na wengine hudanganya kwa namna yoyote ile kwa lengo la kujipatia kipato.
TFDA inakiri tatizo kubwa la matumizi ya vipodozi vyenye kemikali hapa nchini licha ya kutoa elimu kwa njia mbalimbali ikiwamo kwenye mihadhara na maonesho kama vile ya wakulima Nane nane, Sabasaba na mengine.
Matumizi ya vipodozi vyenye viambata sumu yanazidi kuteketeza nguvu ya Taifa kutokana na ongezeko la ugonjwa wa saratani, hivyo ni jukuu la kila Mtanzania kumwelimisha mwenzake ili kuepukana na ongezeko hilo.
Pia serikali inapaswa kuhakikisha inaongeza kipengele cha vipodozi na madhara yake katika mitaala ya mafunzo kwa shule za msingi na sekondari ili kuhakikisha janga hilo linapungua na kutokomea kabisa.
Hakuna maoni