Mhadhiri chuo kikuu mbaroni kwa kumkashfu rais Dk. Magufuli
Idadi ya watu
wanaokamatwa kwa tuhuma za kumkashfu Rais John Magufuli kupitia mitandao ya
kijamii imezidi kuongezeka baada ya polisi kumkamata Mhadhiri wa Chuo Kikuu
Kishiriki cha Elimu cha Mkwawa (Muce), Dk Oscar Magava (48).
Dk Magava amekuwa mtu wa
kumi kukamatwa na polisi katika kampeni za jeshi hilo kudhibiti uhalifu chini
ya sheria ya uhalifu wa mtandaoni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Iringa, Julius Mjengi alisema Dk Magava alikamatwa akiwa Sumbawanga na
alirudishwa mkoani Iringa.
Mjengi alisema Septemba
15, mwaka huu walipata taarifa kuwa mhadhiri huyo anatumia mitandao ya kijamii
kumkashfu Rais. Alisema waliamua kumsaka na walipopata taarifa kuwa Dk Magava
amekwenda Sumbawanga waliwasiliana na polisi wa huko wakamkamata na kumrudisha
Iringa.
Hata hivyo, Kamanda
Mjengi hakuyataja maneno aliyotumia Dk Magava kumkashfu Rais kwa madai kuwa
bado wanaendelea na uchunguzi na kwamba ukikamilika atafikishwa mahakamani.
Kamanda Mjengi
aliwatahadharisha wananchi kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii kwa
kuitumia kwa ajili ya maendeleo na si kutukana wala kukashfu viongozi au watu
wengine.
Watu mbalimbali wamekuwa
wakikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kumkashifu Rais au jeshi la
polisi.
Mwisho
Hakuna maoni