Breaking News

Wanafunzi afya waitupia lawama wizara

WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imejikuta lawamani ikidaiwa kuwanyima namba wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya afya wanaofanya wanaofanya mitihani ya mwisho na wanaoendelea.
Wakizungumza jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, wawakilishi wa vyuo kadhaa walisema wazazi na wanavyuo wamekuwa wakilalamikia hatua hiyo.

“Hatua hii imechukuliwa na Kitengo cha Mafunzo Wizara ya Afya kwa madai kwamba wanafunzi wamechelewa kulipia mitihani hiyo,” alisema mmoja wa wawakilishi hao akiomba kutotajwa jina gazetini.
Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi stadi, Joyce Ndalichako

Wawakilishi hao walitoka katika vyuo vya St. Aggrey Mbeya, Musoma COTC, Sengerema, Tandabuhi cha Mwanza, Royal Pharmacy na Chuo cha KAM cha Dar es Salaam.
Wote walikiri kuwa vyuo vinatambua kuwapo kwa tarehe ya mwisho ya kupeleka majina ya waliolipia mitihani.
“Kwa hali ilivyo si Watanzania wote wenye uwezo wa kulipa ada hiyo miezi minne kabla ya wakati; huwa ni ngumu sana. Wizara ilitaka malipo yakamilishwe Aprili, miezi minne kabla ya mitihani yenyewe,” alisema mmoja wao na kuongeza:
"Mfano wa usumbufu tunaoupata ni wanafunzi wa Chuo cha Tandabuhi waliosafiri hadi kwenye vituo vya mitihani mikoa mbalimbali walikopangiwa na wizara lakini wakakuta hawana namba. Huu ni usumbufu mkubwa.
Wawakilishi hao walishangaa wizara kushindwa kutoa muda mrefu kwa wanafunzi kufanya malipo wakati vyuo vingi hufanya hivyo.
Imefahamika kuwa wanafunzi wengi walilipia mitihani yao kati ya miezi miwili na mitatu kabla, lakini wizara imekataa kuwapa namba wakidaiwa kuchelewa.
 “Tunaomba serikali itambue kwamba Watanzania wa kawaida kipato chao ni cha shida. Unakuta mzazi ana watoto zaidi ya wawili, wote wanasoma.
“Mgogoro wa vyuo na Kitengo cha Mafunzo Wizara ya Afya ni wa muda mrefu. Vikao mbalimbali vimekaa chini ya NACTE, mawaziri na uongozi lakini hakuna suluhu,” alisema mdau mwingine.
Wadau hao walimtaja Naibu Mkurugenzi wa kitengo hicho, Dk. Bumi Mwanasege, kama kikwazo kwa wamiliki wa vyuo.

 Chanzo: Raia Tanzania

Hakuna maoni