Rais Magufuli atuma salamu za rambirambi-ajali New Force
LEO Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi
kwa familia zilipatwa na msiba kufuatia ajali ya basi la Kampuni ya New Force iliyotokea
jana tarehe 19 Septemba, 2016 majira ya saa 2:00 Usiku katika Kijiji cha
Lilombwi, Kata ya Kifanya, Tarafa ya Igominyi Mkoani Njombe ambapo watu 12
wamepoteza maisha na wengine 28 kujeruhiwa.
Basi
hilo limepinduka katika kona ya barabara wakati likisafiri kutoka Dar es Salaam
kwenda Songea Mkoani Ruvuma.
Basi la kampuni ya New Force likiwa limepinduka |
Katika
salamu hizo kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Rehema Nchimbi, Rais
Magufuli amesema amepokea taarifa za ajali hiyo kwa masikitiko makubwa na
kwamba anaungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki wote waliopatwa na msiba
katika kipindi kigumu cha majonzi.
"Ndugu Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Rehema Nchimbi
naomba unifikishie pole nyingi kwa wote walipatwa na msiba, wamewapoteza
wapendwa wao, wamewapoteza watu waliowategemea na hakika familia zimetikisika.
"Sote tuwaombee wote waliofikwa na msiba wawe na moyo
wa subira, uvumilivu na ustahimilivu na pia tuwaombee Marehemu wote wapumzishwe
mahali pema peponi, Amina" Amesema Rais Magufuli.
Rais
Magufuli pia amewapa pole majeruhi wote na amewaombea wapone haraka ili waweze
kuungana na familia zao na kuendelea na shughuli zao za kila siku.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar
es Salaam
20
Septemba, 2016
Hakuna maoni