Mgawanyo keki ya taifa uonekane kwenye miradi ya maendeleo
Na Komba kakoa
KUSHINDWA kupeleka fedha zinakohitajika kutoka hazina ni moja ya changamoto iliyokwamisha utekelezaji wa bajeti zilizopita.
Kwamba ni jambo lililokwamisha utekelezaji wa miradi mingi inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
MAKAMU wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu, leo Januari 5, 2016 amezindua miradi ya maendeleo katika mkoa wa Geita |
Ni wazi kwamba katika kila bajeti ya serikali, kuna fedha za mishahara pamoja na za matumizi mengine ambazo zinapaswa kufika kwa wakati, kwa lengo la kuwezesha rasilimali watu kutekeleza majukumu ya maendeleo kwa wananchi.
Wakati watu wakilipwa mishahara ili watekeleze majukumu yao, ikiwamo usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, inashangaza kuona fedha za kutekeleza miradi hiyo ambayo inawagusa wananchi moja kwa moja kushindwa kufikia walengwa kwa wakati.
Inaelezwa kuwa njia mojawapo ya kugawa keki ya taifa kwa wananchi, ni kupitia kwenye miradi ya maendeleo ambayo huwagusa wao moja kwa moja.
Taarifa zinaeleza kuwa katika bajeti ya mwaka 2015/16, Wizara zote hazikupata fedha za maendeleo kwa asilimia 100, kwani nyingi ziliishia asilimia 80, huku nyingine zikikosa kabisa.
Katika bajeti hiyo zilitengwa Sh. Trilioni 5.92 za miradi ya maendeleo, lakini hazikufika, huku za matumizi mengine zikiwa ni Sh. trilioni 16.57 ambazo zilikwenda kwa wakati.
Katika bajeti ya mwaka huu wa fedha tuliouanza Julai Mosi, fedha za maendeleo zilizotengwa ni Sh. Trilioni 11.8 ambayo ni asilimia 40 ya bajeti ya Sh. Trilioni 29.539 ya mwaka huu, ikiwa ni fedha nyingi kuelekezwa kwenye eneo hilo tofauti na bajeti zilizopita.
Fedha za maendeleo ndizo zinatafsiri ya bajeti kwa wananchi wa kawaida kwa kuwa haitoshi kumweleza mwananchi kuwa serikali imepanga kukusanya na kutumia kiasi hiki kwa mwaka huu wa fedha kama hazina tafsiri ya moja kwa moja kwa maisha ya kawaida.
Tafasri ya bajeti na mgawanyo wa keki ya taifa unaonekana kwenye miradi ya maendeleo kama ya elimu, afya kwa mwananchi kwenda kwenye vituo, zahanati na hospitali na kupata huduma bora.
Katika miradi ya maji ambayo mwananchi atapata huduma hiyo umbali wa mita 400 kama ilivyoelezwa katika Ilani ya mwaka 2015 ya Chama Cha Mapinduzi, kadhalika kwenye miundombinu bora ambayo itamuwezesha mwananchi kusafirisha mazao yake kutoka shambani kuyafikia masoko na kusafiri kwa ajili ya shughuli nyingine, kutoka eneo moja kwenda jingine.
Hivyo, ili tafsri hiyo ionekane kwa wananchi hao ni lazima fedha za maendeleo ziende kwa wakati na thamani ya fedha ionekana kwenye miradi husika, ili kuwa na maendeleo endelevu yanayotajwa na kufikia malengo ya kuwasaidia watanzania maskini kuondokana na hali hiyo.
Iwapo fedha za miradi zitaendelea kuchelewa ni wazi kuwa mwaka mpya wa fedha utafika na wananchi wataona ni mazoea yale yale ya kutowasaidia kubadilisha maisha yao.
Hivyo, Kama serikali imepanga kiasi fulani kwa maendeleo ni vyema kikaenda kwa haraka kama ilivyo kwenye mishahara ya nguvu kazi ya kusimamia utekelezaji wa miradi husika.
Bajeti zilizopita licha ya kuwa na fedha kiduchu za maendeleo huku fedha nyingi zikielekezwa kwenye matumizi mengine, bado zilichelewa kufika na kusababisha miradi mingi kushindwa kutekelezwa, hali iliyowafanya wananchi kutoona tafsiri ya bajeti.
Mwananchi wa kawaida hahitaji kuona takwimu kubwa za fedha ambazo hazipo mfukoni mwake, anahitaji kuona tafsiri hiyo kwenye huduma muhimu za kijamii, zinazogusa maisha yake moja kwa moja na hivyo kumrahisishia shughuli za uzalishaji ambao utachangia katika ukuaji wa uchumi.
Haitakuwa na maana iwapo nguvu kazi itapata malipo yake kwa wakati na huku kazi wanayofanya haina mafanikio kwa kuwa hakuna fedha za kutekeleza, na hivyo kuwa na bajeti ya kulipa mishahara na matumizi mengine zaidi, kuliko kuzielekeza kwenye miradi ya maendeleo ya wananchi wa kawaida.
Tunahitaji kubadilisha maisha ya wananchi na inawezekana kupitia miradi ya maendeleo, hivyo ni vyema serikali ikahakikisha fedha zilizotengwa zinakwenda kwa wakati na siyo kuwa na bajeti hewa ambayo haitekelezeki.
Mara kwa mara wabunge wamepaza sauti zao kuieleza serikali iache kuwa na bajeti hewa au ambayo inashindwa kiakisi uhalisia, kwa kuelekeza fedha kiduchu kwenye maendeleo, na huku nyingi zikifanya shughuli zisizo na matokeo chanya kwa wananchi husika.
Takwimu za serikali zinaeleza mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 6.1 hadi 5.6, na licha ya takwimu hizo, bado hazina tafsiri ya haraka kwa maisha ya mwananchi wa kawaida, kwa kuwa hali ya maisha imezidi kuwa ngumu na huduma za jamii zikiendelea kuwa hafifu siku hadi siku.
Hivyo, tunahitaji kuona utekelezaji wa bajeti unakuwa na tafsiri ya haraka kwenye maisha ya wananchi kwa fedha za miradi ya maendeleo kupelekwa kwa wakati.
Hakuna maoni