Walimu wanolewa kuhusu KKK, Na Mwandishi wetu, Bukoba
Walimu
wa shule za msingi wamehimizwa kujenga na kuimarisha stadi za kusoma, kuandika
na kuhesabu (KKK) kuongeza umahiri wa wanafunzi na mabadiliko chanya.
Hayo
yalisisitizwa mwishoni mwa wiki na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya
Uongozi wa Elimu (ADEM) Bagamoyo, Dk. Siston Mgula, wakati wa ufunguzi wa
mafunzo kwa walimu wa darasa la tatu na nne kutoka wilaya za Kyerwa na Missenyi
mkoani Kagera.
Dk.
Mgula aliwataka walimu hao kuwaimarisha wanafunzi ili stadi hizo ziweze
kuwajenga katika kujitegemea na kuleta mabadiliko chanya kwao na kwa taifa.
Akimkaribisha
Dk. Mgula, mratibu wa mafunzo hayo, Bernard Merumba, alisema walimu 388 wapo
tayari kwa mafunzo hayo.
“Hii
ni awamu ya mwisho ya mafunzo kwa walimu wa Mkoa wa Kagera na tayari walimu
1,770 tayari wamepata mafunzo,” alisema.
Hadi
mwisho wa programu hiyo, walimu 23,000 nchini watakuwa wamehudhuria mafunzo
hayo na kutunukiwa vyeti.
Mwenyekiti
wa mafunzo, Mwalimu Anatoria Joram wa Shule ya Msingi Ishunju wilayani
Missenyi, alimuahidi Dk. Mgula ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mafunzo hayo
kuwa watayatumia maarifa waliyopata kwa manufaa ya taifa na kuyapeleka pia kwa
wenzao ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Hakuna maoni