Breaking News

Wazazi waweza kujengea watoto misingi ya afya



Na Mwandishi Wetu

KUHAMASISHA watoto wako kula vyakula sahihi, kufanya mazoezi na kupunguza muda wa kuangalia televisheni kunaweza kusitoshe kuwajengea tabia za kuimarisha afya. Pia unahitajika kuongoza kwa mfano, watafiti wanashauri.

"Ingawa mchango wowote ambao wazazi wanaweza kutoa ni mzuri, tumegundua watoto wana nafasi kubwa zaidi ya kushika miongozo kama wazazi watakuwa wanatenda wanayoasa," anasema mwandishi wa utafiti huo, Dk. Heather Manson.

 Hilo linamaanisha kuwachukua wanao na kwenda nao uwanjani kucheza, kuweka vyakula salama kiafya vipatikane kwa urahisi na kudhibiti muda wa kukaa kwenye televisheni, anasema Manson, mkuu wa kitengo cha uhamasishaji afya, magonjwa sugu na udhibiti wa majeraha katika Shule Kuu ya Afya ya Ontario nchini Canada.
 Katika nchi za Marekani na Canada, mtoto mmoja kati ya watatu ni menye uzito kupitiliza au mnene kupita kiasi, hivyo kuwa katika hatari ya kupata matatizo makubwa ya kiafya. Madaktari sasa wanajua kuwa kuishi kiafya kunajumuisha si tu kutembea zaidi, bali kukaa muda mfupi zaidi -- kujihusisha na masuala machache yanayofanya mtu akae mahali pamoja kama kuangalia TV au kuingia mtandaoni, watafiti wansema.
Kwa ajili ya utafiti huu mpya, watafiti waliwapigia simu zaidi ya wazazi 3,200 wenye angalau mtoto mmoja mwenye umri wa chini ya miaka 18 kwenye jimbo la Ontario. Wazazi waliulizwa juu ya tabia zao kuhusiana na muongozo wa kitaifa wa mazoezi ya mwili, milo yenye afya na muda muafaka kuangalia TV.
Nchini Canada, watoto wenye umri kati ya miaka 5 mpaka 17 wanashauriwa kufanya mazoezi ya kutoka jasho kwa angalau dakika 60 kwa siku. Kutegemeana na umri na jinsia, kanuni zinashauri kula milo minne mpaka 8 ya matunda na mbogamboga kwa siku. Kuhusu muda wa burudani ya kutazama TV, si zaidi ya saa mbili ndiyo mapendekezo.
Watafiti waligundua kuwa wazazi ambao huwapeleka watoto wao katika maeneo ambayo wanaweza kujishughulisha kimwili, kama viwanja vya kuchezea na kwenye programu za michezo, walikuwa na mara mbili ya uwezekano wa kuripoti kuwa watoto wao wametimiza matakwa ya muongozo wa michezo kuliko wale ambao hawakupeleka.
Wazazi ambao walishiriki katika michezo hiyo na watoto wao walikuwa na asilimia 35 zaidi ya uwezekano wa kuripoti kuwa watoto wao walifikia malengo, kulinganisha na wale waliokaa nje ya viwanja.
Aidha, wazazi ambao waliwezesha watoto wao kula matunda na mbogamboga katikati ya milo mikuu mitatu ya siku walikuwa na uwezekano mara tano zaidi wa kuripoti kuwa watot wao wametimiza matakwa ya muongozi wa lishe, utafiti uligundua.
Msisitizo katika mlo wa pamoja kama familia na kupunguza kutazama TV kulisaidia, pia.
Wazazi ambao walikuwa nyumbani lakini mbali na TV walikuwa na uwezekano wa asilimia 67 zaidi kusema watoto wao walikula matunda na mbogamboga za kutosha. Na wazazi ambao waliweka masharti katika kuangalia TV, 'tablets' na vifaa vingine vya kielektroniki walikuwa na nafasi mara mbili zaidi ya kuripoti watoto wao walifuata kanuni za kupunguza matumizi ya kuangalia vitu hivyo kwa siku.
"Mambo yote haya yanahitaji jitihada za mzazi," Manson anasema, na anaeleza zaidi kuwa matokeo yake yanalipa ugumu unaoweza kuonekana.
Matokeo ya utafiti huo yanaendana na ambacho Stephanie Quirantes, mtaalamu wa lishe wa jumuiya, aligundua katika programu zake kwenye Hospitali ya Watoto ya Nicklaus jijini Miami. Moja inaandikisha vijana matipwatipwa na mama zao. "Tunataka kina mama hao wajifunze juu ya mazoezi ya mwili na lishe," Quirantes alisema.
Kuongoza kwa mfano kunalipa, alisisitiza.
"Haitoshi kusema, 'Fanya hivi,'" Quirantes anasema. Wakati vijana wanapoona mama zao wanafuata tabia njema kiafya, inawahamasisha wao, pia. Matokeo yanaonyrsha "tunaelekea kwenye uelekeo sahihi kwa ambacho tunafanya," Quirantes anasema.
Kuwa na karoti na matunda kwenye jokofu nyumbani kunasaidia.
"Kuwa na vitafunwa hivi tayari tayari," alisema, ili watoto waweze kuchukua tu wakati wakienda mazoezini michezoni au kucheza baada ya muda wa masomo. "Watoto hawatomenya wenyewe matunda," anasema.
Quirantes anasema faida zake ni kwa pande zote mbili. Kina mama wanaoshiriki na mabinti zao mara nyingi huboresha tabia zao wenyewe kiafya, amegundua.
Makala hii ni kwa mujibu wea jarida la HEALTHDAY

Hakuna maoni