Waliochoma moto shule kukiona-Na Mwandishi wetu - MAELEZO
SERIKALI
imesema itawachukulia hatua kale wote watakaobainika kwa sababu moja au
nyingine kuhusika na matukio ya moto yaliyotokea mkoani Arusha hivi karibuni.
Hayo
yalisemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia,
Profesa Simon Msanjila katika mahafali ya tano ya Shule ya Msingi ya Macedonia
iliyopo Tabata Segerea jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Akizungumza
kwa niaba ya Profesa Msanjila, Mkurugenzi wa Elimu ya Msingi wa wizara hiyo,
Sarah Mlaki, alilaani matukio hayo.
Alisema
mbali na kuwachukulia hatua wahusika, Serikali imechukua hatua mbalimbali
kudhibiti majanga ya moto katika shule za sekondari za bweni nchini.
Jengo
la shule ya sekondari Njombe likiwaka moto baada ya kuchomwa na wanafunzi
|
“Tutachukua
hatua stahiki kwa wale ambao watabainika kwa sababu moja au nyingine wanahusika
na majanga hayo,” alisema Mkurugenzi Mlaki.
Mkurugenzi
huyo aliongeza kuwa Serikali pia imejipanga kuboresha miundombinu ya shule zake
ili watoto Watanzania wapate haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Kwa
upande mwingine, Mlaki alisema soko la vitabu vya kiada vinavyotumika katika
shule za msingi nchini limevamiwa na watu mbalimbali na Serikali inafahamu kuwa
kuna vitabu vingine havina ubora unaostahili kwa matumizi ya shule.
Alisema
Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TEA) imepewa dhamana ya kuandaa
vitabu vya kiada ili wanafunzi wote kutumie vitabu hivyo bila ya kuwa na
tofauti katika elimu inayotolewa.
“Ninaamini
tatizo hilo litatatuliwa kadri siku zinavyokwenda kwa kuwa taasisi husika
tayari inalishughulikia kulingana na uzito wake,” alisema.
Katika
mahafali hayo, jumla ya wanafunzi 53 wa shule hiyo walihitimu na wanatarajia
kufanya mitihani ya taifa ya darasa la saba mwaka huu, wakiwemo 24 wanaume na
wanawake 29.
Mwalimu
Mkuu wa shule hiyo Shukuru Mbwire alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2009,
imekuwa ikifanya vizuri katika mitihani ya darasa la saba na la nne ambapo
ilianza na wanafunzi 70 lakini hadi sasa ina wafanuzi 782.
Alisema
katika matokeo ya mitihani ya kitaifa ya darasa la saba shule hiyo imekuwa
ikifanya vizuri mwaka hadi mwaka ambapo katika mitihani ya mwaka 2015 shule
hiyo ilipata wastani wa daraja A na kushika nafasi ya 3 kati ya shule 56
kiwilaya, nafasi ya 28 kati ya shule 534 kimkoa na kitaifa ilishika nafasi ya
219 kati ya shule 16,096.
Hakuna maoni