Tathmini ya Athari kwa Mazingira ifanyike haraka
Na Komba Kakoa
JUNI 5 mwaka Watanzania waliungana na mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Mazingia Duniani ikiwa ni kutekeleza azimio la Stockholm ambalo lilipitishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa la mwaka 1972.
Wakati wa mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa uliohusu Mazingira huko Stockholm, nchini Sweden iliamuliwa kuwa kila ifikapo tarehe hiyo kila mwaka iwe ni Siku ya Mazingira Duniani.
Aidha, siku hiyo pia lilipitishwa azimio la kuunda Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia Mazingira Duniani, (UNEP), ambapo tangu wakati huo, nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania zimekuwa zikiadhimisha siku ya Mazingira Duniani kila mwaka ikiambatana na ujumbe maalumu unaotolewa na Umoja wa Mataifa.
Inaelezwa kwamba madhumuni ya maadhimisho ya Siku hiyo ni kutoa fursa kwa jamii duniani kutambua na kuwa na uelewa wa pamoja wa masuala yahusuyo Mazingira.
Pia kuhamasisha watu wa jamii mbalimbali kushiriki kikamilifu kwenye maadhimisho haya na pia kuwa mstari wa mbele katika kuchukua hatua za kuhifadhi na kulinda Mazingira, kutoa fursa kwa jamii kufahamu kwamba wao wana wajibu wa kuzuia madhara na mabadiliko hasi katika Mazingira.
Kimataifa, mwaka huu maadhimisho hayo yanafanyika nchini Angola ambapo inaelezwa kuwa maamuzi ya kupeleka maadhimisho hayo Angola ni kutokana na maazimio ya nchi ya Angola ya kupamabana na biashara haramu ya Meno ya Tembo na Pembe za Faru.
Kauli mbiu iliyoongoza maadhimisho haya kimataifa ilikuwa “Go Wild For Life” ikimaanisha kuhamasisha jamii kuchukua hatua madhubuti na za makusudi ili kulinda maisha ya wanyamapori kwani wanaunda sehemu muhimu ya mazingira yetu.
Kwa upande wa Tanzania Wizara ya Maliasili na Utalii, pamoja na wadau wengine hapa nchini na kote duniani, wanaendelea na jitihada za kulinda wanyamapori nchini.
Aidha rais wa awamu ya tano John Pombe Magufuli aameazimia kushinda vita dhidi ya ujangili wa aina zote .
Mbali na kauli mbiu ya kimataifa lakini ya Kitaifa hapa kwetu ilikuwa `Tuhifadhi Vyanzo vya Maji kwa Uhai wa Taifa letu. Maji ni Uhai wa Binadamu, ni Uhai wa Wanyama Pori, na ni Uhai wa Uchumi wa Taifa kwa ujumla’
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba anasema wameamua kutumia kaulimbiu hiyo kutokana uharibifu mkubwa wa Vyanzo vya Maji hapa nchini, ambapo sehemu kubwa ya maeneo ya vyanzo vya maji yanatumiwa kwa namna ambazo si endelevu kwa kilimo.
“Shughuli nyingi za kijamii zikiwemo uchimbaji madini, ufugaji, ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni, mkaa na ujenzi na nyingine nyingi husababisha kupungua kwa mtiririko wa maji katika mito mingi nchini katika kipindi cha takriban miongo mitano iliyopita,” anasema.
Kutokana na hali hiyo inaelezwa kwamba baadhi ya mito imebadilika na kuwa ya msimu, kuchafuliwa sana na mingine kukauka hivyo ni dhahiri kwamba bila kupambana na uharibifu wa vyanzo vya maji na mito, mito yote mikuu hapa nchini, kama vile Rufiji, Pangani, Ruaha na mingineyo, ambayo inategemewa sana kwa uhai na ustawi wa Watanzania wengi itakauka ndani ya miaka 15 ijayo.
“Kaulimbiu hiiya kitaifa inahamasisha jamii kushiriki kikamilifu kuhifadhi vyanzo vya maji kwa kutofanya shuguli za uharibifu kwenye vyanzo vya maji hivyo shughuli pekee ambazo tunatakiwa kuzihamasisha ni kupanda miti kwenye maeneo yanayozunguka vyanzo hivyo na kupiga marufuku shughuli zinazoharibu vyanzo vya maji,”.
Makamba ambaye ni mbunge wa jimbo la Bumbuli (CCM) anatoa wito kwa taasisi, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wananchi wote kushiriki katika kusimamia na kuhakikisha vyanzo vya maji vinahifadhiwa ili binadamu na wanyamapori waendelee kuishi,”.
Mbali na hivyo pia kumekuwepo na udhaifu katika uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira, kwa sehemu kubwa, Sheria ya Mazingira inatekelezwa katika ngazi za Serikali za Mitaa.
Kutokana na hali hiyo Makamba anasema Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI pamoja na mamlaka nyingine inakamilisha utengenezaji wa Sheria Ndogo za Mazingira pamoja na Kanuni zake ili kuhakikisha kwamba Sheria ya Mazingira inatekelezwa kwa ukamilifu wake.
“Kuna shughuli za uwekezaji ambazo zinahitaji kufanyiwa Tathmini za Athari kwa Mazingira (Environmental Impact Assessment), hivyo kwa wote watakaobainika kuwa hawakufanya wataadhibiwa,”
“Hivyo tunatoa muda wa miezi miwili, hadi tarehe 1 Agosti 2016, kwa wale ambao hawana Vyeti vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira katika shughuli zao waende Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanyiwa Ukaguzi wa Mazingira (Environmental Audit). Shughuli zinazohusika ni zile ambazo zimeorodheshwa kwenye Sheria ya Mazingira ya 2004, kuanzia kifungu cha 81 - 103 na Kanuni zake za mwaka 2005,” anasema.
Hakuna maoni