Breaking News

Same wapinga hukumu ya Mahakama--Na Mwandishi Wetu, Same


 WANANCHI wa Kitongoji cha Mkanyeni, Ruvu Mferejini Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, wameandamana hadi Mahakama ya Ardhi wilayani hapo kupinga hukumu iliyotolewa na mahakama hiyo kumpa ushindi mwekezaji aliyevamia eneo lao.
 Wakizungumza wilayani humo wiki iliyopita, wananchi hao walimuomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kuingilia kati mgogoro huo auliodumu kwa miaka miwili ili kuepuka umwagaji damu unaoweza kutokea.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Kata ya Ruvu Mferejini, Mathayo Songoi, alisema ardhi hiyo ya eneo la Mkanyeni lenye ukubwa wa hekari 644.4 ni mali yao ya kiasili.

 Alisema baba na mama yake walizaliwa katika ardhi hiyo yenye miundombinu bora kwa wakulima na wafugaji tangu mwaka 1958 lakini katika hali ya kushangaza, mwaka jana alijitokeza mtu na kudai kuwa eneo hilo ni mali yake.
 “Mtu huyu anayejiita mwekezaji wala hana nyaraka zozote zinazoonyesha kuwa eneo hilo ni mali yake,” alisema Songoi.
 Alidai kuwa hakuna kikao chochote cha kijiji kilichopitisha muhtasari wa kumkabidhi mwekezaji huyo aliyejulikana kwa jina la IBIS International, lakini katika hali ya kushangaza mwekezaji amewashitaki wananchi Baraza la Ardhi kwa mada ya kuvamia eneo lake.
Bibi kizee mwenye umri wa miaka 100 ambaye naye alishiriki maandamano hayo, Maria Abrahamu, alisema yeye alizaliwa katika ardhi hiyo na wazazi wake ambao wameshatangulia mbele ya haki.
 Kikongwe huyo alisema kwa sasa hajui hatima ya maisha yake baada ya mahakama kumpa ushindi mwekezaji huyo kutokana na makazi yake kuwa ndani ya ardhi hiyo.
 “Naiomba sana serikali kutusaidia kutupa haki yetu kwa sababu hutujui ni wapi kwa kwenda kuishi kwa sasa tumekuwa tukija hapa mahakamani kila kunapokucha lakini kilio chetu hakisikilizwi,” alisema Bibi Maria.
 Mwananchi mwingine, Grace Mshana, alisema mwekezaji huyo amekuwa akiwanyanya na kuwatishia maisha kwa silaha za moto, akidai kuwa hakuna mtu wa kumwajibisha.
Alisema miaka yote wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali katika eneo hilo lakini katika hali ya kushangaza, mwaka jana akaibuka mwekezaji huyo na kudai kuwa eneo hilo ni mali yake na kuanza kuharibu miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba ya eneo hilo.
 Karani wa Mahakama hiyo aliyekataa kutaja jina lake, aliliambia gazeti hili kuwa anachokifahamu ni kuwa kesi hiyo imehukumiwa na aliyeshinda ni mwekezaji.
Chanzo:Raia Tanzania


Hakuna maoni