Mvua zijazo na majanga yake
Na Mwandishi wetu
MAMLAKA ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA), imetoa taarifa ya kuwapo mvua kidogo zitakazonyesha kwa kiwango
chini ya wastani, ambayo kitaalam zinaitwa ‘La Nina.’
Mvua hizo katika lugha ya
kawaida na hawa kwa wakulima zimezoeleka kama ‘Mvua za Vuli’ au ‘za kupandia’
na zinatarajiwa kunyesha kuanzia mwezi ujao, Novemba na Desemba.
Kulia Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzania (TMA) Joyce Kijazi akiwa na Mkurugenzi wa Utabiri Hamza Kabelwa. |
Dk. Agnes Kijazi, anasema
kitaalam mvua hizo zimepewa majina tofauti kama vile ‘El Nino’ kwa mvua kubwa. Mvua
hizo ziliwahi kunyesha nchini mwaka 1990.
“Unajua wataalam walitupa
jila la ‘El- Nino’ wakati zilinyesha mvua nyingi, lakini kwa sasa wamesema tena
kunapotokea mvua za chini ya wastani katika msimu wa mvua wanasema zinaitwa ‘La
Nina,” anasema Dk. Kijazi.
Mkurugenzi huyo anasema,
wakati sehemu nyingi za nchi zinatrajiwa zisipate mvua kwa kiwango
kinachotarajiwa, isipokuwa maeneo ya pembezoni mwa Ziwa Victoria na Kusini mwa
nchi.
Dk. Kijazi anasema katika
kipindi hicho cha miezi mitatu aliyoitaja, matarajio ni mvua kuanza mwezi ujao
katika ukanda wa Ziwa Victoria na baadhi ya maeneo ya mikoa ya Pwani na Kaskazini
mwa nchi.
KWA NINI MVUA?
Dk. Kijazi anasema hali hiyo
ya joto, inaashiria kuwapo upepo wenye unyevunyevu hafifu kutoka Mashariki, kuelekea
Pwani ya Afrika Mashariki.
Pia, anasema kuongezeka joto la
baharini, jirani na pwani nchi ya Angola, hususan katika miezi hiyo mitatu,
inachangia kuwapo upepo wenye unyevu kuanzia ukanda wa Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo (DRC), hadi Kusini-Magharibi ya Tanzania.
Dk.Kijazi anasema hali hiyo inaelezwa
kusaidia kupunguza matukio ya vimbunga nchini.
HALI YA BAADAYE
Dk. Kijazi anasema, bado hali
ya mvua si kitaifa salama sana. Maeneo mengi yanatabiriwa kuwa na upungufu wa
mvua katika siku zijazo.
Kutokana na hilo, mkurugenzi
huyo wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), anasema kuna uwezekano wa
kutokea athari katika sekta mbalimbali, pamoja na kuathiri utekelezaji wa
majukumu zake.
Anataja sekta husika kuwa za Kilimo
na Usalama wa Chakula, Nishati, Afya, Maji na ofisi zinazohusika na Mamlaka za Miji
na Menejimenti ya Maafa.
Hali ngumu ya upatikanaji
mvua inatarajiwa kuleta ugumu katika ustawi wa mazao ya kilimo katika maeneo
mengi nchini, kutokana na mtiririko mdogo wa maji.
Dk. Kijazi anaongeza kuwa,
vina vya mito na mabwawa nchini vinatarajiwa kupungua kutoka katika hali yake
ya kawaida ambayo imezoeleka.
Anasema ni mazingira
yanayoendana na hatari ya kutokea mlipuko
wa magonjwa katika baadhi ya maeneo nchini, chanzo kikuu kikiwa ni uhaba wa
maji safi na salama.
USHAURI KWA WAKULIMA
Dk. Kijazi anasema mvua za
kutoridhisha katika miezi, kunahatarisha mazao na malisho ya mifugo.
Ushauri wake kwa wakulima ni
kwamba, waandae mashamba na pembejeo mapema na kwa kuzingatia ushauri wa maofisa
ugani wa kilimo, kuhusu matumizi sahihi ya ardhi na mbegu.
Jingine wanaloshauriwa
wakulima ni kutumia kwa uangalifu akiba ya chakula na kuangalia namna ya kulima
mazao yanayohimili hali ya hewa ya kipindi hicho.
Matumizi hayo yanahusu
kuzingatia
kilimo cha umwagiliaji na
kuzalisha mazao ya chakula ya muda mfupi.
Katika maeneo yanayokabiliwa
na upungufu wa malisho na maji ya mifugo na wanyama pori, Dk. Kijazi anawashauri
wakulima wa maeneo hayo kuhifadhi chakula kwa ajili ya malisho ya mifugo.
Ubashiri wa Dk. Kijazi
kuhusiana na athari ni uhaba wa mvua utaosasabisha uhaba wa malisho, utaibua migogoro
baina ya wakulima na wafugaji, katika maeneo wanayoishi jirani.
Anatoa ufafanuzi kwamba, ni
jambo linaloweza kuharibu mimea ya kilimo na kuleta ukosefu wa chakula cha
kutosheleza.
Katika hilo, Dk. Kijazi
anashauri mamlaka zinazosimamia wanyamapori na jamii, iishio katika maeneo hayo
kuchukua hatua stahiki dhidi ya migogoro inayoweza kujitokeza katika maeneo
mengi ambayo huenda yakakumbwa na mvua.
Anasema mamlaka zinazosimamia
huduma za utalii na uhifadhi za wanyamapori zinapaswa kuchukua hatua madhubuti,
ikiwamo kuzuia uharibifu wa miundombinu hususan barabara na madaraja, yaliyomo ndani
ya hifadhi.
MAMLAKA ZA MIJI
Dk. Kijazi ambaye ametoa
tahadhari katika maeneo mengi kulingana na usalama wa hali ya hewa, anawasihi
wananchi
wahakikishe wanaweka mifumo bora
wa njia za kupitisha maji katika kipindi cha mvua.
Anasema kuna uwezekano wa
kuwapo mvua nyingi ndani ya kipindi kifupi, hivyo ni muhimu kutolewa tahadhari
kutoka kila upande wa nchi kuhusiana na mwenendo huo wa mvua.
Kwa mujibu wa Dk. Kijazi ni
kwamba, hata katika baadhi ya maeneo ambako kunakadiruwa kuwapo mvua za kipindi
kifupi, kunaweza kuwapo mvua nyingi katika kipindi kifupi.
Anasema kutokana na uhaba wa maji
safi na salama ambayo ina atahri kubwa katika shughuli za kibinadamu katika
kipindi hicho, wananchi wanashauriwa kuchukua hatua za kujihadhari kupitia
matendo yao.
Dk. Kijazi anaikumbusha Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuchukua tahadhari ya kuchukua
hatua zinazotakiwa kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.
Mkurugenzi wa TMA anatoa rai
kwa wanahabari na vyombo vyao kusaidia kutoa taarifa sahihi kwa wananchi,
kuhusu mwenendo wa mvua katika kipindi
hicho chote.
Pia anawaomba wananchi
kujenga tabia ya kufuatilia kwa makini taarifa zinazohusu hali ya hewa, ili
kujihadhari kwa kadri inavyopaswa.
@Nipashe
Hakuna maoni