Breaking News

Elimu haiwezi kupiga hatua masilahi ya walimu yasipozingatiwa



Na Komba Kakoa

                           RIPOTI ya taasisi ya Twaweza ya tathimini ya elimu kwa  watoto ya mwaka 2014 imebaini udhaifu mkubwa  wa wanafunzi wa darasa la saba jambo ambalo ni dhahiri kuwa hali hiyo inatishia maendeleo ya elimu hapa nchini.
Kupitia mradi wake wa uwezo, Twaweza wanasema kuwa wanafunzi wanne kati ya kumi wa darasa la saba sawa na asilimia 44 hawawezi kusoma hadithi kwa lugha ya Kiingereza ya kiwango cha darasa la pili.

Wawili kati ya 10  ambayo ni sawa na asilimia 16 kadhalika hawawezi kusoma hadithi ya Kiswahili ya kiwango cha darasa la pili. Pia wawili kati ya 10 sawa na asilimia 23 hawawezi kufanya hesabu za kuzidisha za kiwango cha darasa la pili.
wanafunzi wa darasa la kwanza wakiwa darasani

Meneja wa mradi huo, Zaida Mgalla anasema kuwa watoto 32,694 walipimwa katika  masomo hayo kutoka kaya 16,013 za wilaya 50 za Tanzania Bara katika jumla ya shule za msingi 1,309 za nchini humo.
“Tulilenga kuwapima watoto wenye umri kati ya miaka saba hadi 16 kupitia wakusanya takwimu wa kujitolea 2,626 ambao walikuwa wakitathmini watoto hawa...katika utafiti wetu tulibaini kwamba watoto kutoka familia zenye uwezo hasa mjini wana uwezo mkubwa zaidi wa kupata stadi za msingi za kusoma na kufanya hesabu kuliko wenzao wanaotoka familia masikini au wanaoishi vijijini,”alisema.
Mgalla anasema pamoja na mafanikio yanayoonekana kwenye ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi, Tanzania bado haijatimiza dhamira yake iliyojiwekea ya mpango wa ya elimu bure kwa wote kutokana na kukosekana kwa usawa kwenye vifaa vya shule, mazingira mazuri ya kujisomea, uandikishaji na matokeo ya kujifunza.
Anasema juhudi za kuhakikisha kuwa watoto wanaelewa vizuri wawapo darasani sio tu katika kununua madawati au ujenzi wa madarasa bali ni uwekezaji katika idara ya walimu kwa kulipwa madai yao yote pamoja na kuboreshewa mazingira yao ya kazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze anasema kuwa kamwe elimu haitaweza kupiga hatua iwapo masilahi ya walimu yasipozingatiwa.
“Popote pale uendapo,  kama waalimu hauwathamini hakuna kusoma, hivyo wadau wana wajibu wa kushirikiana na serikali ili kuwaboreshea mazingira mazuri walimu hao,”anasema.
Katika ripoti hiyo, imeelezwa kuwa matokeo ya masomo yote matatu yaliyopimwa na tathmini ya uwezo ya mwaka huo yameendelea kuwa chini.
Katika ripoti hiyo asilimia 54 ya wanafunzi wa darasa la tatu ndiyo wanaoweza kusoma hadithi ya Kiswahili ya darasa la pili. Kuhusu hadithi ya Kiingereza asilimia 19  ya wanafunzi wa darsa hilo ndiyo wanaoweza kusoma hadithi  kwa lugha hiyo kwa kiwango cha darasa la pili na asilimia 35 pekee wanaweza kufanya hesabu za darasa la pili.    
Mgalla anasema katika kipindi cha miaka mitano ya tathmini ya mradi huo, kumekuwa na mabadiliko finyu kwenye matokeo ya kujifunza na kusema kuwa viwango vya ufaulu wa somo la Kiswahili vinaonyesha matokeo chanya.
“ Kwa mfano mwaka 2012 na 2014, idadi ya wanafunzi wa darasa la tatu ambao wanaweza kusoma hadithi ya Kiswahili ya darasa la pili imeongezeka kutoka asilimia 26 hadi 54,” anasema
Kuhusu tatizo la utoro anasema nusu ya asilimia 19.2 ya watoto ambao hawakuwa shuleni walionaika kwenye utafiti huo wanatoka kwenye kaya masikini.
Pia anasema kuna utofauti kubwa kati ya mkoa mmoja na mwingine katika idadi ya watoto wenye umri wa miaka saba hadi 16 ambao hawapo shuleni ambapo asilimia 8 ya watoto wanaotoka mkoani Dar es Salaam wenye umri wa miaka 7 hadi 16 hawapo shuleni ikilinganishwa na asilimia 35 wa mkoa wa Shinyanga.
Kwa upande wa mazingira ya shule, ripoti imebainisha kuwa utoro wa walimu umekuwa ni tatizo sugu ambalo linalowaumiza watoto katika kujifunza.
Kwa mwaka 2014,  asilimia 31 ya walimu hawakuwa shuleni wakati tathmini hiyo inapita ikilinganishwa na mwaka 2012 ambapo ilikuwa asilimia 21.
Aidha kuhusu uwiano wa wanafunzi na walimu nao ni tofauti ; wanafunzi 126 kwa mwalimu mmoja katika mkoa wa Mara na wanafunzi 56 kwa mwalimu mmoja katika mkoa wa Pwani.
Kwa upande wa vitabu, ripoti inaonyesha kuwa wanafunzi 26 kwa kitabu kimoja mkoani Tabora na wanafunzi watatu kwa kitabu kimoja mkoani Mtwara, Kilimanjaro, Katavi, Ruvuma na Njombe.
Kwa upande wake, Meneaja Mkuu wa mradi huo wa Uwezo Afrika Mashariki, Profesa John Mugo anasema kuwa matatizo ya kielimu kwa nchi za ukanda huo yanafanana ingawaje kuna utofauti kidogo.
Anasema kuwa kwa nchi ya Kenya, walimu ambao hawafiki darasani ni asilimia 11 tu ikilinganishwa na Tanzania yenye kiwango cha asilimia 31 ya utoro wa walimu kazini.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi ya Nsongwanhala iliyopo Nzega , George Mgina, anasema kuwa katika ripoti hiyo, changamoto nyingi zimeonekana huku kubwa zaidi likiwa ni utoro wa waalimu jambo ambalo kwa namna moja au nyingine limesababisha wanafunzi kushindwa kufanya vizuri licha ya kupewa masomo rahisi wakati wakiwa katika ngazi za juu.
”Bila ya Mwalimu hakuna shule, hakuna kusoma wala kujifunza, kwa hiyo suala hili lisipoangaliwa kwa makini, elimu yetu bado itasalia kuwa shakani huku mataifa jirani yakiendelea kutupita,”anasema.
Moja ya wasomi mahiri na wachambuzi wa masuala ya elimu nchini, Profesa wa chuo kikuu cha Dar es Salaam, Kitila Nkumbo, anaunga mkono hoja ya walimu kutopewa stahiki zao kwa wakati jambo ambalo linasababisha kuwepo kwa matokeo hasi kwa wanafunzi wengi.
Anasema kuwa elimu si bahasha, bali ni uwezo wa mwanafunzi katika kuhakikisha anapanukia kiuelewa na kifikra, kuwa na mawazo thabiti na yenye nguvu ambayo yanayoweza kuwa kichocheo katika maendeleo.
“Kuweka dawati zuri, vitabu vizuri haikidhi kuonyesha kuwa ndiyo umemaliza jitihada za kuboresha elimu, daima mwalimu ndiyo nguzo katika kitivo hicho cha elimu, hivyo anastahili kuangaliwa kwa umakini zaidii,”anasema.
Utafiti huo ni wa tano sasa, kutoka mwaka 2010 hadi 2014 , lengo kuu likiwa  ni kuangalia kiwango cha watoto katika kuwapima kujifunza kinadharia na vitendo kwa ajili ya ustawi wa Taifa.
Ingawaje Twaweza wamekuwa wakijitolea katika kufanya tafiti hizo, matunda yake bado yanaonekana kulega kutiliwa mkazo na serikali hasa katika suala zima la mahitaji ya walimu hivyo jitihada za ziada zinahitajika ili kulikomboa taifa letu dhidi ya adui aitwaye ujinga kama ambavyo Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kunukuliwa katika moja ya hotuba zake enzi ya uhai wake.
“Tuna maadui watatu, ujinga, umasikini na maradhi, tunapaswa kupambana nao ili kuwashinda,”alinukuliwa Hayati Mwalimu Nyerere katika moja ya hotuba zake.

Hakuna maoni