Yaliyomkuta mkandarasi wa Uwanja wa Taifa Dar
Na Mwandishi wetu
*Alijenga
chini ya kiwango, akanyongwa na Serikali ya China?
UWANJA wa Taifa uliopo jijini Dar es Salaam ni moja kati ya viwanja bora kabisa vya michezo barani Afrika, ukiwekwa nafasi ya pili kwa uzuri na gharama nyuma ya ule wa Soccer City uliopo Afrika Kusini.
Kwa Afrika Mashariki, uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watu 60,000 waliokaa unashika nambari moja ukivipiku viwanja maarufu kama Kasarani cha Kenya na Namboole Nelson Mandela kilichopo Mukono nje kidogo ya jiji la Kampala, Uganda.
Balozi wa China nchini, Dk. LU Youqing |
Mara baada ya kumalizika kujengwa kwa
uwanja huo na kukabidhiwa serikalini mwaka 2008, kumekuwapo tetesi kwamba
mkandarasi aliyesimamia ujenzi huo aliujenga chini ya kiwango na hivyo
kuikasirisha Serikali ya China iliyotoa fedha nyingi katika mradi huo.
“Wachina hawana mchezo na fedha zao, huyu
aliyejenga uwanja huu aliporudi kwao akashitakiwa na kunyongwa. Sisi tunaona
bonge la uwanja kumbe haujakidhi vigezo,” alisikika akisema shabiki mmoja wa
soka ndani ya uwanja huo hivi karibununi.
Raia Tanzania lilifanya juhudi za
kuufahamu ukweli wa suala hilo ambalo limeingia sana vichwani mwa Watanzania kujua
sababu hasa za kunyongwa au kuadhibiwa kifo kwa mhandisi huyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wiki
iliyopita, mmoja wa maofisa wa Kampuni ya Beijing Construction Engineering
Group ya China, alikanusha kuadhibiwa au hata kukamatwa kwa msimamozi yeyote wa
mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Taifa.
“Ni uvumi tu wa mitaani. Uwanja huu
ulisimamiwa na wahandisi watatu na walipomaliza, walirejea China,” alisema
ofisa huyo akiomba kutoandikwa gazetini kutokana na taratibu za kampuni hiyo,
huku akishauri pia majina ya wahandisi hao yasiandikwe hadi baada ya kupata
kibali kutoka makao makuu ya kampuni.
Kampuni hiyo inamilikiwa na Serikali ya Mji wa Beijing, ikijihusisha na ujenzi wa
barabara, majumba makubwa, kufunga vifaa mbalimbali, usafirishaji, ujenzi na
usanifu wa majengo.
Beijing Construction Engineering Group ni
kundi la kampuni zipatazo 190 zikitoa ajira kwa zaidi ya watu 20,000 maeneo
mbalimbali duniani.
Raia Tanzania liliambiwa na ofisa mmoja wa
Ubalozi wa China nchini kuwa wasimamizi hao waliporejea nyumbani walitunukiwa
tuzo mbalimbali na mmoja kati yao kwa sasa amechukuliwa na kuajiriwa
serikalini.
Kwa ujumla, kampuni hiyo alipewa tuzo ya
juu unayotolewa kila mwaka kwa kampuni iliyofanya vyema inayofahamika nchini
China kama RUBAN kutokana na mradi huo.
“Ndio maana ninasema hakuna ukweli wa mtu
kuhukumiwa sababu ya kuboronga ujenzi wa Uwanja wa Taifa. Uwanja ulijengwa kwa
viwango vilivyotakiwa.
“Miongoni mwa kazi bora zilizowahi
kufanywa na kampuni hii ni mradi wa Uwanja wa Taifa na baada ya kumalizika,
tulipata kazi katika miradi mingine mikubwa ya kitaifa na kimataifa. Mengineyo ni
upotoshaji mtupu,” alisema ofisa huyo wa ubalozi.
Taarifa zaidi zinadai kuwa China hakuna
sheria ya kunyonga watu kwa makosa ya mradi kutekelezwa kwa kiwango cha chini.
Ofisa wa Beijing Construction Engineering
Group aliyezungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam alisema katika
utekelezaji wa mradi huo, mbali na ajira kwa Watanzania, kampuni pia ilichinba
visima kama msaada kwa jamii inayozunguka eneo la mradi, ilijenga barabara na
kuwafundisha Watanzania wengi usanifu na ujenzi.
“Mradi ulipokamilika, wengi walipata ajira
kwenye kampuni nyingine kutokana na ujuzi tuliowapa. Hii yote ni michango yetu
kwa Watanzania,” alisema.
Kama ishara ya kukubalika kwa kazi
waliyoifanya, kampuni hiyo ilipewa miradi mingine kadhaa nchini baada ya Uwanja
wa Taifa ikiwemo ujenzi wa Chuo Kikuu cha Sheria kilichopo Lshoto, Chuo Kikuu cha
Dodoma, majengo ya Benki Kuu mjini Dodoma na sasa wanajenga Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Ujenzi wa Uwanja wa Taifa ulianza mwaka 2004
na Rais wa China, Hu Jintao akakabidhi ufungua wake kwa Rais Jakaya Kikwete mwaka
2008 baada ya ujenzi kukamilika.
Gharama za mradi huu ilikuwa Dola 60,000,000
ukitekelezwa na wataalamu 1,000 kutoka China huku ukitoa ajira kwa Watanzania 5000.
“Wakati mradi ukikabidhiwa kwa Tanzania mwaka
2008, Serikari ya Tanzania ilisema kwa wakati huu haina wataalamu na vifaa vya
kukarabati uwanja huo ukiharibiwa au vifaa kuharibika wakati wa matumizi ya
kawaida.
“Kwa hiyo wataalamu wa Kichina wa kampuni
iliyoujenga waliendelea kuhudumia Uwanja wa Taifa, gharama zote za kitaalamu na
ufundi zililipwa na Serikali ya China hadi Julai 2013 pale Balozi, Dk. Lu Youqing
aliposaini mkataba na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Michezo kuukabidhi rasmi kwa
serikali,” alisema.
Chanzo:Raia Tanzania
Chanzo:Raia Tanzania
Hakuna maoni