Wanasiasa wasemeeni wakulima pia
SHUGHULI
kubwa ya kiuchumi kwa Watanzania walio wengi nchini, kimsingi ni kilimo.
Na kwa hali
hiyo, si kupotoka nikisema kwamba walio wengi nchini ni wakulima.
Hii ni kwa
sababu, kilimo ndiyo shughuli ya kiuchumi inayotegemewa na wananchi wengi
wanaoishi vijijini.
Kwa mujibu
wa takwimu za Sensa ya Mwaka 2012, asilimia 70 ya Watanzania milioni 45
wanaishi vijijini, huku asilimia 30 wakiishi mijini.
Kwa hali
hiyo, serikali inaposisitizwa itoe kipaumbele kibajeti kwenye eneo la kilimo,
ni kwa misingi kuwa, maendeleo yake yanagusa Watanzania wengi.
Kwamba serikali
inapowekeza kwenye kilimo, inakuwa imewekeza kwa takribani asilimia 70 ya
wananchi wake.
Mkulima |
Na uwekezaji
kwenye eneo hilo unajulikana, kwa maana ya huduma anazozihitaji mkulima, kuwa
ni pamoja na mbegu bora, zipatikane kwa bei nafuu na kwa wakati.
Mkulima
anahitaji mbolea, awezeshwe kutoka kwenye jembe la mkono, aanze kutumia la
kukokotwa na mifugo ama mashine kama matrekta.
Anahitaji
dawa za kuua wadudu wamazao, ama kwa ajili ya palizi.
Anahitaji
wataalamu wa kilimo ili azalishe kwa tija.
Anapovuna,
aweze kupata soko la mazao yake, kama ni pamba, korosho, kahawa, mpunga,
mahindi na mengineo.
Na kutokana
na mabadiliko ya tabianchi ambayo yameathiri hata uhakika wa mvua kwenye baadhi
ya maeneo, mkulima anahitaji miundombinu ya umwagiliaji, ili aweze kuwa na
uhakika wa maji kwa karibu kipindi chote cha mwaka.
Kimsingi uwekezaji
wa kumwezesha mkulima apate huduma zote hizo, ndio unaotakiwa kwake.
Kwa bahati
mbaya uwekezaji katika sekta hii umekuwa ukifanyika, lakini si kwa kiwango cha
kuwawezesha wakulima wetu wafanikiwe.
Na ndiyo
maana bado kuna kilio cha miaka mingi kutoka kwa kundi hili la wananchi,
linalounda asilimia 70 ya Watanzania wote.
Kilio cha
ukosefu wa mbegu bora, karibu katika maeneo yote ya nchi.
Kwa mfano
katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kumekuwa na kilio cha wakulima wa
zao la pamba kutoka kanda ya ziwa cha kuuziwa mbegu ‘feki’zilizosababisha wakakosa
mavuno.
Na mbaya
zaidi wanasiasa walitajwa kuwa nyuma ya kadhia hiyo, wakidaiwa kushiriki
kuzipigia upatu, mbegu hizo kuwa ni mbegu bora.
Aidha kuna
kilio cha wakulima wengi katika mikoa ya Rukwa, Ruvuma na hata ile ya Mtwara na
Lindi, ya kucheleweshewa mbolea na dawa za kuua wadudu.
Lakini hata
pale zilipofika kwa kuchelewa, bado bei yake ilikuwa ni ya ghali.
Aidha kuna
kilio cha siku nyingi cha wakulima kukosa soko la uhakika la mazao yao, lakini
pia mazao yao yakinunuliwa kwa bei ya chini isiyowawezesha kupiga hatua kubwa
za kimaendeleo.
Kwa mfano
katika mikoa ya Rukwa na Ruvuma, wakulima wanazalisha mahindi lakini si yote
yananunuliwa.
Kwamba hata Wakala
wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), anakosa bajeti ya kutosha kununua
mahindi yote yanayozalishwa na wakulima.
Lakini pamoja
na changamoto zote zinazoikumba sekta hii nchini, Muungwana anasikitishwa na
kitendo cha moja ya wadau wa kundi hili, kutowasemea kama wanavyofanya kwa
makundi mengine ya kijamii kama lile la wafanyabiashara.
Wadau ambao
anawashangaa Muungwana kwa kukaa kwao kimya bila ya kusemea kwa mapana,
changamoto hizi za wakulima kama wanavyofanya kwa kundi la wafanyabiashara ni
wanasiasa, na hasa wale wa upinzani.
Ukiangalia kwa
mfano kwenye sakata la mizigo bandarini na kwenye sekta ya utalii, lililotokana
na hatua ya serikali kuanzisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), wanasiasa wa
upinzani wamejitokeza kwa nguvu zote kulisemea.
Sasa sijui
kwa sababu linawagusa wafanyabiashara!
Ni rai ya
Muungwana kwa wanasiasa, na hasa wa upinzani, kuwa na
kifua pia cha kuwasemea na wakulima pia.
Mwisho
Hakuna maoni