UKATILI-Mwanafunzi asimulia alivyoteswa na walimu
NI
ukatili. Hilo ndilo neno lililokuwa likitumika kuelezea mkasa uliohusisha
kipigo alichokipata mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari
Mbeya Day, Sebastian Chinguku.
Akizungumza
na Nipashe kwa mara ya kwanza jijini humo jana, ikiwa ni baada ya kupata nafuu
kufuatia tukio hilo lililozua mjadala mkali bada ya video yake kusambaa kwenye
mitandao ya kijamii, mwanafunzi huyo, alisema amefarijika kutokana na hatua iliyochukuliwa
na Serikali dhidi ya walimu waliomfanyia ukatili huo ambao kamwe hakuutarajia.
Walimu hao walioonekana kwenye video iliyotikisa kwenye mitandao ya kijamii
kuanzia juzi, wakimpiga Chinguku, ni Frank Msigwa na John Deo, amabo ni wanafunzi
wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam, (Duce) na Sanke Gwamka wa
Chuo cha Ualimu cha Mwalimu Nyerere. Wote walikuwa katika mafunzo ya vitendo.
Mwanafunzi aliyefanyiwa Ukatili, Sebastian Chinguku |
Hata
hivyo, Chinguku alielezea kusitikishwa kwake na hatua iliyochukuliwa dhidi ya Mkuu
wa Shule, Magreth Haule.
Akizungumza
na Nipashe jana muda mfupi baada ya kutoka katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa
Mbeya, Chinguku alisema hatua ya Serikali ya kuwavua ualimu wahusika wa ukatili
huo ni sahihi kwa sababu kipigo walichompa kilihatarisha maisha yake na siyo
kwa nia ya kumfundisha kama ilivyo dhamira ya walimu wengine.
“Kwakweli
walimu wale walionekana kama walikuwa na dhamira ya kuniua kutokana na kipigo…
hawakuwa na utaratibu. Walikuwa wakinipiga popote pale kwa kutumia fimbo,
mateke, ngumi na makofi huku wakiniburuza chini,” alisema na kuongeza:
“Wakati
wakifanya hivyo, walisistiza kuwa wao wamepitia JKT (Jeshi la Kujenga Taifa) na
hivyo siwezi kuwababisha… nashukuru niko hai. Naishukuru pia Serikali kwa hatua
ilizochukua.”
Akieleza
kuhusu adhabu aliyopewa mkuu wa shule ambaye amevuliwa madaraka, Chinguku
alisema hana mamlaka ya kuzuia, lakini anaamini kuwa hastahili kaudhibiwa kwa
tukio hilo kwa sababu upo uwezekano kuwa baadhi ya walimu walimficha
kilichotokea kwa sababu hakuwapo na ndiyo maana hakuchukua hatua.
CHANZO
CHA KIPIGO
Akisimulia
chanzo cha kufanyiwa ukatili huo, alisema kuwa ni kisasi walichokuwa nacho
walimu hao dhidi yake kutokana na hisia kwamba yeye ni mjeuri, hasa kutokana na
ukweli kuwa tayari alishakorofishana na mmoja wao kabla ya siku ya tukio.
Akisimulia
zaidi, Chingukwa alisema kuwa siku ya Ijumaa, Mwalimu Msigwa alitoa zoezi
lakini yeye hakuwapo shuleni siku hiyo na hivyo akashindwa kufanya kazi iliyotolewa
naye (Mwalimu Msigwa).
Alisema
baada ya hapo, ilipofika Jumatatu, mwalimu huyo (Msigwa) alifika darasani na
kuamuru wale wote ambao hawakufanya kazi aliyotoa wapite mbele. Akawatandika
wote fimbo tatu kila mmoja.
Alisema
ilipofika zamu yake ya kuadhibiwa, yeye alijaribu kujitetea kuwa hakuwapo siku
hiyo ya kutolewa kwa kazi hiyo.
Alisema
jibu hilo halikumridhisha mwalimu ambaye alimshika na kwenda naye ofisini
ambako walimu wengine waliokuwa kwenye mazoezi ya vitendo walikuwamo na kuanza
kumpiga hovyo kwa fimbo, ngumi na mateke.
Alidai
kuwa awali, mmoja wa walimu hao aliwahi kukorofishana naye kutokana na
kuamuriwa avue sweta siku ya mtihani lakini yeye akakataa kwa kujitetea kuwa
anaumwa na ndipo naye akaungana na Msigwa na mwalimu mwingine kumshambulia.
Alisema
wakati akifanyiwa unyama huo, walimu wengine waajiriwa walikuwa kwenye ofisi
nyingine wakifanya kikao, hivyo hawakujua kilichokuwa kikiendelea.
Alisema
kuwa baadaye aliambiwa na Makamu Mkuu wa Shule hiyo aandike barua ya kuomba
msamaha kwa kosa la kuwapiga walimu, jambo ambalo alidai hakukubaliana nalo
lakini baada ya kutoa maelezo aliambiwa aandike barua ya kueleza tukio
lilivyokuwa na ndicho alichokifanya.
Hivi
sasa, mwanafunzi huyo anaendelea vizuri kiafya baada ya kupata matibabu
kufuatia kuvimba baadhi ya maeneo mwilini na pia kuwa na jeraha karibu na jicho.
BABA
ANENA
Baba
wa mwanafunzi huyo, John Chinguku, ambaye ni mfanyakazi wa benki tawi la Mbozi,
alinena mazito kwa kudai kuwa hadi sasa ni kama haamini kuwa mwanawe bado yuko
hai kutokana na kipigo hicho cha walimu wake.
Akizungumza
na Nipashe jana, Chingukwa alisema alistushwa mno baada ya kupata taarifa
kupitia picha za video za ‘whatsapp’.
Hata
hivyo, alisema ni jambo la kumshukuru Mungu kwamba mwanawe yuko hai kwa kuwa
kipigo kilichokuwa kinaendelea kilihatarisha maisha yake.
Alisema
ameridhishwa na hatua zilizochukuliwa na serikali hadi sasa na kusisitiza kuwa
walimu wanapaswa kuzingatia weledi wa kazi zao na siyo kuadhibu watoto kwa
namna ile aliyofanyiwa mwanawe.
“Mimi nafanya kazi Mbozi na mama yao hawa
vijana yupo Dar es Salaam, anamuuguza kaka yao ambaye anasumbuliwa na mguu,
lakini pia pale nyumbani kwangu sina umeme ndiyo maana sikuweza kuwasiliana
nao, lakini naishukuru Serikali kwa kuchukua hatua za haraka maana ile video
inaonyesha wale walikuwa na makusudi mabaya,” alisema Chinguku.
Alisema
baada ya kufuatilia fomu namba tatu (PF3) na kumchunguza kijana huyo ilibainika
kuwa anaendelea vizuri.
MAWAZIRI
WALIVYOINGILIA
Juzi,
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, aliiambia
Nipashe kuwa amelazimika kumvua madaraka mwalimu Mkuu wa shule hiyo pamoja na
walimu ambao walifanya kitendo hicho baada ya kupata undani wa kilichotokea.
Prof.
Ndalichako alisema baada ya kuona video ya walimu hao mtandaoni, aliwatuma Wadhibiti
wa Ubora wa Shule Nyanda za Juu Kusini, Mbeya kulifuatilia na ndipo akachukua
hatua hiyo.
Prof.
Ndalichako alisema adhabu aliyopewa mwanafunzi huyo ni kinyume cha maadili ya
kazi.
“Nimeongea na mwalimu mkuu wa shule hiyo
ananiambia alikuwa hajui tukio hilo, nilimuuliza kama yeye ni mkuu wa shule
kweli, yaani tukio kama hili linatokea shuleni kwake hajui hadi analishuhudia
kwenye mitandao ya kijamii,” alisema.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba,alisema waliofanya tukio hilo
watasakwa ili hatua zichukuliwe dhidi yao.
Waziri
wa nchi ofisi ya Rais Serikali za Mitaa na Tawala za mikoa (Tamisemi), George
Simbachawene, naye alitangaza kumshusha cheo Mwalimu Mkuu kwa kufumbia macho
kitendo hicho na kutotoa taarifa mpaka video ilipozagaa mtandaoni.
Mwisho
Hakuna maoni