BAWATA: Chanzo cha waganga matepeli ni mfumo
Na
Komba Kakoa
BARAZA
la Waganga wa Tiba Asili (BAWATA) limeiomba serikali kupitia Wizara ya Afya Kitengo
cha tiba asili kuboresha mfumo wa usajili wa dawa ili waweze kubaini matapeli wanaovamia taaluma
hiyo huku wakijifanya wana uwezo wa kutibu.
Kwamba
mfumo wa usajili ukiboreshwa wataweza kutengeneza umoja utakaosaidia kufanya kazi
kwa umoja na kuimarisha tiba asili hapa
nchini na hatimaye kusaidia wananchi wanaoteseka
kwa maradhi.
Ombi
hilo limetolewa na Mkurugezi wa Baraza hilo, Islam Makingili alipokuwa akizungumza
na TABIBU kufahamu msimamo na kauli ya baraza hilo kuhusu tuhuma ya utapeli dhidi ya baadhi ya waganga wa tiba
asili.
“Tunachotaka
hapa ni uboreshwaji wa mfumo wa usajili, kwani watu waliopewa jukumu la usajili
hawana utaalamu wa tiba asili, hawana uwezo wa kuwatambua matatibu halisi na matapeli
jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linasababisha matapeli kutumia fedha zao kuvamia
tiba yetu na kuwaumiza wananchi,” alisema.
Katikati ni Makamu mwenyekiti wa Bawata Mohamed Matokeo |
Aliongeza
kuwa wakati umefika sasa shughuli zote za usimamiaji wa tiba asili kwa kila
ngazi kuhusisha waganga wenyewe wa tiba asili kwani wao wana mbinu mbalimbali
za kuwabaini waganga halisi na matapeli kutikana na mfumo wa sasa kuruhusu
kusajiliwa kwa watu wanaojiita waganga wakati hawajui lolote.
Pia
alilalamikia waganga wa tiba asili kusumbuliwa pindi wanapohitaji kumuona mkemia
mkuu wa serikali kwa ajili ya kufanya vipimo vya dawa zao, huku akilalamikia
pia gharama kubwa za usajili wa dawa hizo.
Alidai
kuwa awali gharama za kupima sampuli moja ya miti dawa ilikuwa Shilingi 300
000, lakini kwasasa zimeongezeaka na kufikia Sh. 750,000 kiwango ambacho sio rahisi
kwa matabibu wenye mtaji mdogo kuweza kumudu na kusababisha wengi kuhudumia
wagonjwa bila dawa zao kusajiliwa.
“Katika
kila kijiji, mtaa, kata na wilaya kuna kamati za afya, lengo likiwa ni kusimamia kupitisha fomu watu
wanaoomba uganga, lakini jambo la kushangaza watu ambao hawana taaluma au uwezo
wa tiba asili wanatumiwa kupitisha fomu za maombi ya waganga na kuwa chanzo cha
kusajiliwa watu matapeli kwa kutumia fedha zao,”alisema.
Naye
Mwenyekiti wa baraza hilo, Shaka Mohamed alilalamikia usajili wa dawa kwa njia
ya dola kwamba na kusema kitendo hicho hakijengi uzalendo na kinaathiri ustawi
wa tiba asili hapa nchini.
“Ni
jambo la ajabu sana, kufanyika kwa miamala katika usajili huu kwa njia ya dola,
huu ni uonevu, serikali iingilie kati suala hili ili Tanzania iende sambamba na
mabadiliko ya tiba asili duniani, kwani baadhi ya nchi zimekuwa zikifanya
usajili wa miti dawa bure na katika nchi hizo dawa za asili zimekuwa
zikiyaingizia mataifa hayo fedha za kigeni,”alisema.
Pia
aliishauri ofisi ya mkemia mkuu kutoa ufafanuzi wa matokeo ya vipimo vya dawa
hizo kutokana na mfumo wa sasa huonyesha kiwango cha dawa au kemikali bila
kufafanua madhara, matumizi na faida.
“Waganga wanataka kiwango cha kemikali
kilichomo, kiasi kinachooneshwa kwenye vipimo, kemikali hiyo iko chini au juu,
nini faida au hasara na ushauri wa wa matumizi, sio kuonyesha tu kiwango basi,”alisema.
Hakuna maoni