Bil 18 zatumika utekelezaji miradi ya maendeleo Ilala
ZAIDI ya sh. Bil 18 zimetumika katika utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala katika kipindi
cha miezi sita kuanzia Julai hadi Desemba mwaka 2017
Hayo yalibainishwa jana na Afisa Uhusiano wa Halmashauri hiyo,Tabu
Shaibu, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Afisa Uhusiano-Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Tatu Shaibu akizungumza na vyombo vya habari jana |
Shaibu alisema katika fedha hizo zilizotumika shilingi 8,844,643,432.62
ni mkopo kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya uboreshaji wa barabara zitakazosaidia
kupunguza msongamano wa magari katika barabara za katikati ya mji.
“Barabara zilizoboreshwa kupitia mradi wa DMDP ni ya Olimpio
yenye urefu wa Km 0.68 na hatua ya utekelezaji iliyofikiwa ni asilimia 96.10, Kiungani
Km 0.68 asilimia 85.91, Mbaruku Km 0.38 asilimia 82.58, Kongo Km 0.28 hatua
iliyofikiwa ni asilimia 89.84, Omari-Londo Km 0.53 hatua iliyofikiwa ni
asilimia 84 pamoja na barabara ya Ndanda Km 0.35 hatua iliyofikiwa ni asilimia
86.
Pia Halmashauri imelipa fidia kiasi cha shilingi 3,109,872,121.52
kwa waathirika wa maeneo ambayo yanapitiwa na mradi huo ili kufanikisha
utekelezaji wake.
Aidha, Shaibu alisema katika kipindi hicho Halmashauri imepeleka
jumla ya Shilingi 8,524,000,000 kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo na kiasi kilichotumika
ni shilingi 5,863,659,471
Alisema Halmashauri hiyo imejenga shule mpya nne kutokana na
ongezeko la wanafunzi ambalo limetokana na mpango wa Serikali wa Elimu bila
malipo.
“Shule za Msingi zilizojengwa ni Kidugala iliyopo Kata ya
Chanika, Zavala Kata ya Buyuni, Uamuzi Kata ya Majohe na Kinyamwezi iliyopo Kata
ya Pugu,”alisema Shaibu.
Pia vyumba vya madarasa 28 vilijengwa katika shule za Msingi
Bonyokwa, Mongo la ndege Mbondole, Mji mpya, Kibaga, Bangulo na Misitu na
madarasa sita kukarabatiwa likiwamo moja katika shule Kinyerezi na vyumba
vitano katika shule ya Msingi Mchikichini.
Pia alisema jumla ya matundu ya vyoo yaliyojengwa katika
shule hizo ni 96 na 40 yamejengwa katika shule za zamani ambazo ni Buyuni,
Bwawani, Tungini na Kilimani.
Kwa upande wa Sekondari vyumba 37 vilijengwa katika shule za
Ilala, Halisi, Nguvu mpya, Kerezange, Misitu, Viwege, juhudi, Abbuy Jumaa,
Kisungu, Gerezani, Ugombolwa na Kasulu.
“Halmashauri imejenga vyumba vya madarasa viwili katika
shule ya Sekondari Ilala, Halisi viwili, Nguvu mpya viwili, Kerezange viwili, Misitu viwili, Viwege
viwili, Juhudi 10, Abbuy Jumaa viwili, Kisungu viwili, Gerezani vine, Ugombolwa
vitatu na Kasulu ambayo ni mpya vyumba vine,”alisema Shaibu.
Aidha Halmashauri hiyo imejenga matundu 91 ya vyoo ambayo ni
27 katika shule ya Halisi, Misitu nane, Juhudi 27, Abbuy Jumaa 15, Ugombolwa sita
na 27 kwa shule ya Kasulu.
Aliongeza kuwa pia walifanikiwa kukarabati nyumba ya mwalimu
katika shule ya Sekondari Kimanga sambamba na ununuzi wa samani.
Kadhalika aliongeza kwamba Halmashauri hiyo imechukua hatua
ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi katika shule ya sekondari Mbondole iliyoko
kata ya Msongola kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya usafiri kwa
wanafunzi wanaokaa mbali pamoja na ukarabati wa shule kongwe za jangwani,
Azania na Pugu ambao unaendelea.
Kadhalika alisema wamekamilisha ujenzi wa mradi mkubwa wa
Hospitali ya Mama na mtoto Chanika hivyo kupunguza vifo vya Mama na mtoto pia kupitia
ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam jingo la Mama na Mtoto limejengwa katika
Hospitali ya Amana likiwa na vitanda 100, na kufanya idadi ya vitanda kufikia
353 kutoka 253 hospitalini hapo.
Aliongeza kuwa Halmashauri hiyo imefanya ukarabati wa Majengo
ya huduma za Mama na Mtoto katika Zahanati ya Msongola na Mvuti kwa kutumia
mapatio ya ndani huku ikiendelea kutekeleza ukarabati wa jingo la mapokezi
katika hospitali ya Amana, kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Mbondole, ujenzi
wa magonjwa ya mlipuko katika zahanati ya Kipawa, kukamilisha ujenzi wa
Zahanati ya Lubakaya, kumalizia ujenzi wa Zahanati ya Bangulo
Shaibu alisema katika sekta ya maji halmashauri hiyo imeshaanza
hatua utekelezaji katika miradi ya maji ikiwa ni pamoja na ukamilishaji na
ukarabati wa miradi ya maji katika kata ya Minazi, Tabata, Majohe, Vingunguti,
Sekondari Pugu, Mkera na Pugu Station.
“Ujenzi wa kisima cha maji Mtaa wa Mkera Kata ya Msongola,
ujenzi wa tenki la la ujazo wa kuhifadhia maji kiasi cha lita 250,000 katika
eneo la Pugu Kimani, ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita 150,000 la
kuhifadia maji katika Kata ya Kisukuru pamoja na miundombinu ya usambazaji maji
katika eneo la Kata ya Mzinga,”alisema Shaibu.
Pia ujenzi wa Mradi wa maji Sharifu Shamba kata ya Ilala na
Kata ya Kitunda, Kusambaza mabomba ya maji katika eneo la 511KJ Gongo la Mboto
Jeshini.
Aidha Shaibu aliongeza kwamba katika kipindi hicho
Halmashauri hiyo imepeleka Sh. 543,400,000 kwa ajili ya mikopo kwa wanawake,
vijana na walemavu.
MWISHO
Hakuna maoni