Mechi Dar Kambi Uturuki, hii haiko sawa!!
Na Komba Kakoa
MABINGWA wa Tanzania, timu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam
imeianza vibaya michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika hatua ya makundi,
baada ya kufungwa bao 1-0 na wenyeji wao Mo Bejaia ya nchini Algeria.
Ni dhahiri kwamba Yanga ilijiandaa kisayansi
zaidi kuingia katika mchezo huo na matokeo hayo yametokana na kuzidina mbinu na
waarabu hao ambao hawakuonyesha kiwango cha kutisha sana.
Lakini kwa kujua hali ya hewa ya Algeria kuwa
ni baridi, Yanga waliamua kwenda kuweka kambi nchini Uturuki ambako kuna ya
baridi pamoja na kuendelea na program za kufanya mazoezi usiku, muda
uliolandana sawa na ule ambao mchezo ulipangwa kuchezwa, kweli haya ndio
maandalizi ya kisayansi yaliyofanikishwa na kocha, wachezaji pamoja na benchi
la ufundi.
Ni jambo zuri na lakuigwa kwa timu zetu za hapa
nyumbani kuwa na maandalizi ya hali ya juu ambayo ni ya Kisayansi ili kuweza
kuendana na hali halisi ya upinzani.
Kwamba timu nyingine za Tanzania zinapaswa
kujifunza aina hii ya maandalizi ili kufikia mafanikio pia itakuwa kituko kwa
timu inayojiandaa kwenda kucheza nchi za ukanda wa joto iweke kambi sehemu
yenye baridi. Hii haiku sawa kabisa.
Yanga sasa inajiandaa na mchezo wa pili dhidi
ya TP Mazembe unaotarajiwa kuchezwa Juni 28, katika dimba la Taifa jijini Dar
es Salaam. Nilishtuka nilipopokea taarifa kuwa timu hiyo inaanza safari ya
kurejea Uturuki katika mji wa Antalya kuendelea na kambi yake, nikajiuliza
'Yanga wamesahau nini tena Uturuki?'
Kocha yoyote anapenda mazingira tulivu ili
aweze kuhakikisha mafundisho yake yanawaingia vizuri wachezaji, hii yaweza kuwa
sababu kubwa iliyowafanya Wababe hao wa
mitaa ya Twiga na Jangwani wanogewe na kambi ya Antalya, lakini wamejiuliza
kuhusu hali ya hewa?
Sidhani kama ni sahihi kwa Yanga kuendelea na
kambi ya Antalya wakati wanajua hali ya hewa ya kule ni tofauti kabisa na ya
Dar es Salaam, ambako mchezo unatarajia kuchezwa.
Ingekuwa vyema kama Yanga wangerejea nchini na
kutafuta eneo ama mkoa ambao wanaamini kuna utulivu ikiwezekana kwenda hata
visiwani ambako wamezoea kuweka kambi kujiwinda.
Licha ya mwezi mtukufu wa Ramadhan, Pemba
panabaki kuwa sehemu tulivu na sahihi zaidi kwa Yanga kuelekea kuwavaa Mazembe
ambao wenyewe wameanza vizuri michuano hiyo kwa kuifumua Medeama mabao 3-1
jijini Lubumbashi.
Acha nijifariji kuwa Yanga watapumzika tu pale Antalya kwa siku moja kabla
hawajaanza safari ya kurejea nchini, hawatoweka kambi kama ilivyoelezwa kwavile
kufanya hivyo ni kujiongezea ugumu wa mechi.
Kutokana na uwepo wa mechi jijini Dar es
Salaam, jiji ambalo lina hali ya joto, Yanga wamekosea kuweka kambi Uturuki
ambako kuna hali inayotofautiana na eneo ambalo mchezo unatarajia kuchezwa.
======================
Hakuna maoni